Wacheni mchezo na mtoe pesa za kaunti, magavana waambia Serikali ya Kitaifa
MAGAVANA wa kaunti za ukanda wa Ziwa Victoria (LREB) wameelezea wasiwasi wao kuhusu fedha za mgao kwa kaunti kuchelewa kutolewa, wakitaka Hazina ya Taifa iheshimu katiba na kuhakikisha pesa hizo zinatumwa kwa wakati unaofaa.
Wakiongozwa na Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang’ Nyong’o, magavana James Orengo (Siaya), George Natembeya (Trans Nzoia), Dkt Ochilo Ayacko (Migori), Kenneth Lusaka (Bungoma), Paul Otuoma (Busia), Hillary Barchok (Bomet) na Amos Nyaribo (Nyamira), walielezea mafadhaiko yao katika kongamano lililofanyika Mombasa.
“Tunalia na tunang’ang’ana. Serikali Kuu inakiuka Katiba ambayo inafaa kuheshimu na kutekeleza Sheria ya Ugavi wa Mapato,” alisema Mwenyekiti wa LREB, Prof Nyong’o, akionyesha kukerwa na ucheleweshaji huo.
Kwa mujibu wa Gavana huyo wa Kisumu, kucheleweshwa huku kumelemaza uwezo wa kaunti kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kutimiza majukumu ya kifedha ya bajeti. Alisisitiza kuwa kaunti, tofauti na Serikali Kuu, zinategemea tu mapato yaliyotengwa kupitia Sheria ya Ugavi wa Mapato.
“Mapato ya ndani hayatoshi kukidhi mahitaji ya bajeti za kaunti au kuendeleza huduma muhimu, pamoja na kulipa watumishi wa umma,” alisema.
Alitaja ucheleweshaji huo kuwa “kinyume na katiba,” akisisitiza kuwa ni kosa kuwanyima watumishi wa kaunti mishahara yao, na akailaumu Hazina ya Taifa kwa kudhoofisha uwezo wa kaunti.
Gavana wa Busia, Bw Paul Otuoma, alieleza athari mbaya kwa kaunti za mipakani, akisema kuwa bila fedha hizo, Busia imeshindwa kuendeleza miradi ya uchumi wa majini, uundaji wa ajira, na kukuza utalii katika kaunti hiyo. Magavana hao walitoa wito wa pamoja kwa Hazina ya Taifa kutuma fedha mara moja kwa kaunti.
“Acheni mchezo na mpatie kaunti fedha,” alisisitiza Prof Nyong’o.
Wakati huo huo, magavana hao wanatazamiwa kufanya Mkutano wao wa 12 huko Busia kati ya Novemba 27 hadi 29 mwaka huu. Mkutano huo utaleta pamoja kaunti 14 katika Ukanda wa Ziwa.
“Tunafuraha kuwafahamisha Wakenya rasmi kwamba Kongamano lijalo la 12 la Jumuiya ya Kiuchumi ya Ukanda ya Ziwa litaandaliwa katika Kaunti ya Busia,” alisema Gavana Nyong’o.