Habari za Kitaifa

Malumbano yanukia jamaa anayedai kuwa mwanawe Kibaki akitaka mwili ufukuliwe

Na RICHARD MUNGUTI November 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MALUMBANO makali yanatarajiwa katika kesi ya urithi wa mali ya hayati Mwai Kibaki Juni 26, 2025 kesi iliyoshtakiwa na Jacob Ochola Mwai itakapoanza kusikizwa.

Ochola pamoja na mwanamke anayetambuliwa kwa herufi JNL wamewasilisha kesi mahakamani wakiomba watambuliwe kuwa wana wa hayati Kibaki.

Wawili hao wanaomba Mahakama kuu iamuru mwili wa hayati Kibaki ufukuliwe ufanyiwe ukaguzi wa DNA ibainike ikiwa yeye ni baba yao au la.

Kesi hiyo ya urithi wa mali ya Kibaki ambaye ndiye rais wa tatu kutawala Kenya, ilishtakiwa na Ochola anayedai ni mwanawe kiongozi huyo wa nchi ambaye chini ya utawala wake nchi hii ilistawi mno.

Ochola mwenye umri wa miaka 62 aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu akiomba atambuliwe kuwa mmoja wa warithi wa mali ya kiongozi huyo aliyepata sifa sufufu kutoka kwa uthabiti wa uchumi na ustawi.

Ochola na JNL kupitia kwa mawakili Philip Murgor na Morara Omoke walieleza Jaji Eric Ogolla kwamba watawasilisha maombi ya kupinga kutekelezwa kwa Wosia alioandika Kibaki mnamo Desemba 2016.

Wawili hao walieleza mahakama sahihi katika Wosia huo imeghushiwa.

Kufuatia madai kuwa huenda sahihi iliyo kwenye Wosia huo sio halali, Jaji Eric Ogolla aliamuru mawakili Murgor na Omoke wawasilishe ombi rasmi katika mahakama katika muda wa siku 14.

Pia Jaji Ogolla aliwataka wote wanaohusika katika kesi hiyo watafute suluhu na kuafikiana kuhusu ugavi wa mali ya hayati Kibaki pasi kufukua maiti yake kutwaliwa sampuli kufanyiwa ukaguzi wa DNA.

“Je ninyi mawakili hamwezi patanisha walalamishi na watoto wa hayati Kibaki? Kuna muda wa zaidi ya miezi sita. Tafuteni jinsi mtapata suluhu,” Jaji Ogolla aliwashauri.

Bw Murgor, Omoke na wakili mtekelezaji wa Wosia huo walisema “watajaribu juu chini kufikia suluhu kabla ya Juni 26, 2025.”

Watoto wa Kibaki Judith Wanjiku, James Mark, David Kagai na Antony Andrew Githinji Kibaki wamepinga kesi hiyo ya Ochola wakisema “itakuwa gharama kubwa kufukua maiti ya Kibaki na kuizika tena.”

Watoto wa Kibaki wamesema kwamba watateseka kimawazo iwapo watashuhudia baba yao akifukuliwa na sampuli kukatwa kwa mwili wake.

Wamehoji walikokuwa wawili hao Ochola na JNL kwa miaka yote baba yao alipokuwa hai.

Watoto hao wameuliza sababu ya Ochola kushtaki kesi miaka 60 baadaye.