Anavyogeuza mmea sumu wa Mathenge kuwa vinywaji na bidhaa za kula
DKT Duke Gekonge hakudhania utafiti wake wa PhD kwa mapera ungezalisha Pera Foods, kampuni inayogeuza matunda yasiyothaminiwa kuwa bidhaa muhimu.
Akiwa mwasisi wa Pera Foods, Dkt Gekonge ana shahada ya PhD katika Masuala ya Sayansi ya Chakula na Teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN).
Leo hii, kampuni hiyo aliyoianzisha 2019 iko katika mstari wa mbele kuchakata mimea na matunda yasiyothaminiwa, ikiwemo mmea hatari kwa mifugo – Mathenge, unaojulikana Kisayansi kama Prosopis juliflora.
Pera Foods inaongeza thamani mimea na matunda; kwekwe la bahari maarufu kama sea moss, mkaktusi – cactus, mapera, maembe, ukwaju, mibuyu, haibiskasi (hibiscus) na Mathenge.
Mathenge, mmea wenye miba umekuwa kero hasa maeneo kame (ASAL) ukisemekana kusababisha maafa ya mifugo.
Kaunti ya Baringo, kwa mfano, wenyeji wanakadiria hasara ya mmea huo kuwaangamizia ng’ombe.
Wengi wakiona Mathenge kama mmea hatari, Pera Foods inaona dhahabu.
Safari ya Dkt Gekonge kuongeza thamani Mathenge ilianza alipoungana na Dkt Oscar Koech, Mwanasayansi wa masuala ya ardhi za malisho mwenye uzoefu mkubwa kufanya kazi katika maeneo kame Kenya.
Dkt Koech amekuwa akitafiti mmea huo kwa zaidi ya miaka kumi, akilenga hasa uwezo wake kama chakula cha mifugo wakati wa ukame.
Kulingana naye, maganda ya Mathenge yana protini na sukari nyingi, virutubisho ambavyo ni muhimu kwa mifugo na binadamu.
“Maeneo kame, utapata wanyama wakichangamkia maganda ya Mathenge hususan msimu wa ukame. Ingawa miba yake ni hatari, maganda yana virutubisho vya kutosha,” anaeleza Koech.
Mexico na Amerika Kusini, ambako mmea huu unatoka, maganda yake yametumiwa kwa karne nyingi kama chakula cha binadamu.
Bidhaa za thamani
Ni kupitia ushirikiano wa Dkt Gekonge na Dkt Koech ulizaa maono mapya; kugeuza Mathenge kuwa bidhaa yenye thamani.
Dkt Gekonge, anasema kwa kutumia ujuzi wake wa Sayansi ya Chakula, alianza kufanya majaribio na maganda ya Mathenge ili kutengeneza bidhaa za chakula zinazofaa kwa binadamu.
Matokeo yake ni kuibuka na mtandao wa bidhaa kama mkate, keki, na hata divai.
“Pera Foods huunda vitafunwa na vinywaji kwa Mathenge, na matunda yanayopuuzwa,” anasema Mwanasayansi huyo.
Kampuni hiyo, iliyoanza rasmi shughuli zake 2022, pia inasindika bidhaa za kukabiliana na kupunguza makali ya maradhi kama vile Kisukari na Saratani.
“Bidhaa tunazotengeneza zimeingia sokoni, na kwa sasa tunachakata karibu 25,” Dkt Gekonge akaambia Akilimali wakati wa mahojiano katika kampuni yake iliyoko Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN, tawi la Kabete.
Aidha, alidokeza kwamba hutumia majukwaa ya kidijitali, yaani mitandao ya kijamii kuvumisha soko la bidhaa anazounda.
Kinachofanya Pera Foods kuvutia zaidi ni bidhaa wanazozalisha kutoka kwa mmea wa Mathenge.
Rufas Gachunga, kutoka kitengo cha Sayansi ya Chakula na Lishe UoN, alieleza, “Badala ya kukata na kuangusha miti ya Mathenge, tunaipa thamani. Tunageuza kero yake kuwa rasilimali”.
Mchakato wa kuibuka na bidhaa za mmea huo unahusisha kusaga maganda yake kuwa unga, kisha unachanganywa na viungo vingine kama viazi vitamu na ngano kutengeneza vitafunwa vyenye Protini na afya bora kwa binadamu.
“Unga wa Mathenge una protini nyingi, antioxidants, na virutubisho muhimu mwilini. Tunapunguza hitaji la sukari katika bidhaa zetu kwa kutumia viazi vitamu na ngano, ambavyo pia huongeza thamani ya lishe,” Gachunga aliongeza.
Kibiashara, bidhaa hizo zinateka hela ambapo mkate wa gramu 400 unauzwa Sh60, huku pakiti ya keki sita ikiingia sokoni kwa Sh65.
Divai ya Mathenge kipimo cha mililita 750 kinagharimu Sh1, 500.
Mbali na kutumia majukwaa ya kidijitali, Pera Foods pia inauzia bidhaa zake kwenye hospitali kama Hospitali ya Kitaifa na Rufaa ya Kenyatta (KNH).
“Divai ninauzia wateja moja kwa moja, wanaopendekezwa kwa bidhaa zetu,” anasema Dkt Gekonge.
Isitoshe, amepenyeza soko la kimataifa, akituma shehena ndogo kwenda Amerika, Ulaya, na Asia.
Safari ya Gekonge haikuanza na mmea wa Mathenge.
Anadokeza, awali, alikuwa akilenga matunda yasiyothaminiwa kwa kuyageuza kuwa juisi na bidhaa za tiba.
Ingawa kuanzisha Pera Foods haikuwa rahisi, Gekonge anafichua kwamba ilimgharimu mtaji wa Sh100, 000 na sasa anakadiria biashara yake kuwa yenye thamani ya mamilioni kimawazo.