Habari za Kitaifa

Safaricom motoni kwa kufichua data za wateja wanaoidaiwa kutekwa nyara

Na STEVE OTIENO November 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAKUNDI mawili ya kutetea haki za kibinadamu yameiandikia Safaricom kufuatia ripoti kuwa kampuni hiyo ya mawasiliano imekuwa ikitoa data za wateja wake kwa maafisa wa usalama kuwasaidia kusaka na kuteka nyara washukiwa.

Katika barua yao kwa Mkuu wa Kitengo cha Sera za Umma na Usimamizi wa kampuni Fred Waithaka, Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC) na Kundi la Waislamu kuhusu Haki za Kibinadamu (Muhuri) yalitaja ripoti iliyochapishwa katika gazeti la ‘Daily Nation‘ Oktoba 29, ilionyesha jinsi Safaricom imekuwa ikitekeleza uovu huo.

Makundi hayo ya kutetea haki yaliilaumu kampuni hiyo ya mawasiliano kwa kupeana data kwa maafisa wa polisi “wenye sifa mbaya ya kutumia mbinu haramu kupambana na washukiwa ikiwemo kuwaua.”

Ingawa Safaricom ilitoa taarifa mnamo Oktoba 31, 2024 ikifafanua kuhusu madai hayo, KHRC na Muhuri zinasema taarifa hiyo haikujibu moja kwa moja yale yaliyofichuliwa kwenye uchunguzi huo.

Kwa misingi hiyo, makundi hayo ya kutetea haki za kibinadamu yanaitaka Safaricom kujibu orodha ya madai saba ya “kuchukiza” yaliyotolewa kwenye ripoti ya Daily Nation.

KNHR na Muhuri zilisema kuwa Safaricom inapopewa agizo la mahakama kwamba itoe rekodi za data kuhusu mawasiliano ya simu zinazoweza kuwahusisha maafisa wa usalama na maovu kama mauaji ya kukusudia, hupitisha wajibu huo kwa kitengo cha polisi cha ushirikishi wa umma.

“Hii huleta hali ya mgongano wa kimasilahi kwa kuwapa maafisa wa kitengo kinachotuhumiwa nafasi ya kupata data na kuficha ushahidi kuhusu uhalifu na hatima ya waathiriwa,” mashirika hayo yanasema.

Aidha, yanahoji ikiwa Safaricom ilitoa data ambazo ilithibitisha kuwa halali licha ya kuonyesha dalili kwamba zilivurugwa.

KNHR na MUHURI zinaitaka Safaricom kuthibitisha ikiwa hutoa kwa maafisa wa usalama rekodi hizo za data baada ya kupokea agizo la mahakama kutokana na kesi zinazohusu visa vya watu kutokomezwa na serikali kwa nguvu.

Kwa kukataa kila mara kutoa data muhimu kusaidia katika uchunguzi wa maovu yanayotendwa na serikali nchini Kenya, hata baada ya kupokezwa maagizo ya mahakama, KHRC na MUHURI zinailaumu Safaricom kwa “kuhujumu haja ya kupatikana kwa haki.”

Mashirika hayo pia yanaitaka Safaricom itoe maelezo kuhusu madai kuwa iliruhusu asasi za usalama kupata data za wateja wake hata bila agizo la mahakama, na hivyo kusaidia katika kusaka na kukamatwa kwa washukiwa.

KHRC na MUHURI pia zinataka kampuni hiyo ya mawasiliano kutoa maelezo kuhusu madai kuwa imehifadhi data za “zamani” inazodai ilifuta, zikiwemo data ambazo zinaweza kusaidia katika uchunguzi wa uhalifu uliotekelezwa na serikali.

Mashirika haya mawili pia yanaitaka Safaricom kufafanua kuhusu madai kuwa, pamoja na kampuni ya Neural Technologies Limited, ilitengeneza programu inayowezesha vikosi vya usalama nchini Kenya kupata data za kibinafsi za wateja wao. Na data hizo ndizo zimetumika na maafisa.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga