Wakulima washtuka kugundua ‘zawadi’ ya Rais ilikuwa mkopo
HALI ya kuchanganyikiwa imekumba chama cha ushirika cha wakulima wa kahawa cha Baricho katika Kaunti ya Nyeri baada ya ukaguzi kufichua kuwa msamaha wa deni uliotolewa na serikali miezi miwili iliyopita ni mkopo.
Mnamo Septemba, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi walitembelea chama hicho kuwasilisha ‘zawadi’ kutoka kwa Rais William Ruto.
Bw Oparanya na Bw Wamumbi waliambia wanachama wa chama hicho kinachokabiliwa na madeni kwamba rais aliwapa zawadi ya Sh63 milioni ili kuwaokoa kutoka kwa madeni.
Hii ilikuwa habari njema kwa chama hicho cha ushirika ambacho sasa kinakabiliwa na deni la Sh300 milioni ambalo limerundikana kwa miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, wakulima 7,000 wa kahawa hawakujua kuwa kile ambacho mbunge alikuwa akiita ‘msamaha wa deni’ ni mkopo kutoka kwa serikali!
Mnamo Alhamisi, wakulima walishtuka ripoti ya ukaguzi iliyoagizwa na Bw Oparanya kufichua kwamba ‘zawadi’ hiyo ilikuwa mkopo wa ziada uliotolewa na kampuni ya New KPCU, wa vyama vya ushirika Kenya.
Wakulima sasa wanatakiwa kulipa mkopo huo mpya kwa riba ya kiwango cha asilimia tatu.Wakati wa mkutano maalumu mnamo Septemba 9 mwaka huu katika kiwanda cha kahawa cha Karindundu, Bw Opraranya alisema Rais Ruto aliagiza wizara yake kuanzisha uchunguzi kuhusu madai ya ubadhirifu wa mamilioni ya pesa za wakulima wa kahawa.
Waziri pia aliagiza kamishna wa vyama vya ushirika, David Obonyo, aanze uchunguzi mara moja na kutoa ripoti ndani ya miezi miwili.Wakati wa mkutano huo wa Septemba, alimshutumu aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua kwa kushindwa kurekebisha sekta ndogo ya kahawa kama alivyoagizwa na bosi wake.
“Niliagizwa na rais kuitisha mkutano huu kufuatia kilio cha wakulima. Rais amesikia kilio chenu na serikali imetenga Sh63 milioni kuwasaidia,” Bw Oparanya alisema.
Bw Wamumbi, ambaye aliandamana na mwenzake wa Nyeri Mjini Duncan Maina na Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga, aliwaambia wakulima kuwa amekuja kuwapasha habari njema kutoka kwa Rais.
“Nilifanikiwa kukutana na Rais ambaye amejitolea kuwaondolea wakulima mzigo wa madeni,” alisema.Hata hivyo, ripoti ya uchunguzi iliposomwa kwao Alhamisi wiki hii, wakulima hao walipata mshtuko mkubwa ilipofichuka kuwa chama kinadaiwa Sh300 milioni ikiwa ni pamoja na ‘zawadi’ ya Sh63 milioni kutoka kwa Rais.
Ripoti iliyosomwa na Bw Philip Ouma kutoka afisi ya kamishna wa vyama vya ushirika ilidokeza kuwa chama kinadaiwa na KPCU Sh97 milioni pamoja na Sh63 milioni zinazosemekana kuwa msamaha wa deni.Bw Ouma alisema kuwa kulingana na stakabadhi zilizopo, Sh63 milioni ni sehemu ya mkopo uliotolewa kwa chama na kampuni ya New KPCU.
“Hatuwezi kuamini kile ambacho tumesikia katika ripoti hiyo. Wakati wote, tuliamini kuwa rais alikuwa amefuta deni la Sh63 milioni na hatukuambiwa ni mkopo.
”Kwa nini kutulimbikizia deni bila kutufichulia? Maafisa wa serikali wanawezaje kuwadanganya wakulima? Tumesikitikwa sana,’ alisema mkulima aliyekasirika Gilbert Gicheru.Bw Wamumbi, ambaye hakufika kwenye mkutano huo, hakuweza kupatikana kuzungumzia matokeo ya ukaguzi huo kwa vile hakujibu ujumbe aliotumiwa na mwandishi.
Ripoti ya ukaguzi pia iliangazia madai ya ubadhirifu wa kifedha unaofanywa na baadhi ya maafisa wa chama ikiwa ni pamoja na Sh14 milioni zilizotumiwa kwa ‘uhusiano wa umma’ katika kipindi cha mwaka mmoja.
Imependekezwa kwamba maafisa wa zamani waliopatikana na hatia wafunguliwe mashtaka. Viongozi tisa walisimamishwa kazi na nafasi yao kuchukuliwa na kamati ya muda ili kupisha ukaguzi huo.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA