Mtoto akidhulumiwa mtandaoni huwa anaathirika kisaikolojia
KUNA uwezekano kwamba mtoto anaweza kukutana na watu mtandaoni ambao wanatumia majina na picha sizokuwa zao wakiwa na lengo la kuwashawishi wawe marafiki ili kuwatumia vibaya kwa unyanyasaji na kuwashirikisha katika aina zingine za dhuluma.
Hii ni jambo linapaswa kuwapa wazazi wasiwasi na ni muhimu kuzungumza na watoto kuhusu wanavyoweza kuwa salama.
Wataalamu wa malezi dijitali wanasema kwamba takriban kijana mmoja kati ya watano hutumiwa vibaya na kunyanyaswa wakishiriki mtandaoni hasa kwa kushawishiwa kutuma picha tatanishi.
Katika utafiti mmoja uliofanywa na shirika la kimataifa la Ofcom kuhusu usalama wa watoto wanapotumia mtandao mwaka wa 2021-, asilimia 30 ya watoto wenye umri wa miaka 12-15 walisema walikuwa wamewasiliana na mtu wasiyemjua mtandaoni ambaye alitaka waanzishe urafiki.
“Ni rahisi kujifanya kuwa mtu mwingine kwenye mtandao, jambo ambalo mara nyingi hujulikana kama uigaji mtandaoni. Wakati fulani watoto wanaweza kuishia kutangamana na watu wasio halisi na wenye nia mbaya,” inasema sehemu ya utafiti huo.
Watu hao wamekuwa wakipenya katika makundi ya mitandao ya kijamii au kuunda kurasa za mitandao hiyo wakijifanya kuwa vijana lengo likiwa ni kuwashawishi wawatumie kwa uhalifu.
“Wanaanza kwa kupata uaminifu wa watoto kwa kutumia picha na maelezo feki kuwahusu, kuwapa zawadi na kusema maneno mazuri kwa mtoto,” wanaeleza watafiti hao.
Pindi tu wanapopata imani ya mtoto, huelekeza mazungumzo yao kwa vitendo vinavyokiuka maadili ya watoto kama vile kuwatambulisha kwa ngono kuwauliza kutuma picha za ngono au video zao wenyewe.
Baadaye wanaanza kutisha kusambaza picha hizo au video hizo na familia na marafiki wa mtoto.
Hii ndiyo hufanya watoto kuathirika kisaikolojia na kujipata wametumbukizwa katika vitendo ambavyo hawakutarajia na watu wasiowajua wanaokutana nao katika mitandao.