Habari za Kitaifa

Mswada kunyima wakulima kinga dhidi ya pandashuka za bei ya chai

Na BRIAN AMBANI November 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKULIMA wa majani chai huenda wakakosa ruzuku iliyonuiwa kuwakinga dhidi ya kushuka kwa bei ya chai duniani iwapo Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Majani Chai 2023 utapitishwa.

Mswada huo, ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza Bungeni wiki hii, unakabidhi asilimia 60 ya pesa zitakazokusanywa kutoka kwa ushuru wa majani chai kwa Bodi ya Chai nchini (TBK).

Asilimia 40 iliyobaki itatolewa kwa Wakfu wa Utafiti wa Chai.Ushuru wa asilimia 1 kwa uagizaji na uuzaji wa chai nje ulianzishwa na Sheria ya Chai, 2020. Hata hivyo, ushuru huu haujaanza kutumika baada ya makampuni kadhaa ya chai kwenda mahakamani kutaka utangazwe kuwa ni kinyume na katiba.Kesi mahakamani bado inaendelea.

Hii ina maana kwamba hadi sasa, Bodi ya Chai inaendelea kutegemea kwa kiasi kikubwa ufadhili wa fedha.“Ada ya chai inayokusanywa chini ya kifungu kidogo cha (2) itagawanywa kama ifuatavyo: asilimia sitini itatumika na Bodi katika kuendeleza au kutekeleza kazi au mamlaka yoyote ya Bodi; na asilimia 40 itatumwa moja kwa moja kwa Wakfu wa Utafiti wa Chai kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ya wakfu,” unasema Mswada huo.

Katika Sheria ambayo Mswada unalenga kufanyia marekebisho, asilimia 50 ya kile Bodi ya Chai inachokusanya kutokana na ada hiyo inatumika kwa ajili ya mapato au uimarishaji wa bei kwa wakulima wa majani chai.

Asilimia 15 zaidi inatakiwa kutumika na shirika kwa shughuli zake, asilimia 20 kwa Taasisi ya Utafiti wa Chai na asilimia 15 iliyobaki inatakiwa kutumika kwa maendeleo ya miundombinu katika sekta ya chai.

Mswada huo ulio mbele ya Bunge kwa sasa ulifadhiliwa na Seneta wa Bomet Hillary Sigei na Mbunge wa Konoin Brighton Yegon.Kenya iliuza majani chai ya thamani ya Sh180.57 bilioni mwaka wa 2023, na hivyo kuashiria ongezeko kubwa kutoka Sh138.09 bilioni mwaka uliopita.

Hii ina maana kwamba ikiwa ushuru wa chai ungetumika wakati huo, Bodi ya Chai ingekusanya ushuru wa chai wa Sh1.8 bilioni kutokana na mauzo ya chai nje.Iwapo Mswada huo utapitishwa, ina maana kwamba sasa itakuwa ni uamuzi wa Bodi ya Chai kuamua mapato itakayotengea wakulima wa majani chai.

Mswada huo umeacha Kifungu cha 54 cha Sheria ya Chai, 2020. Sehemu hiyo inaanzisha Hazina ya Chai, ambayo itafadhiliwa na walipa kodi kupitia bajeti, pesa kutoka kwa ushuru wa chai, ruzuku na michango.

Hazina inatakiwa kuleta utulivu wa mapato ya wakulima wa chai.Wafadhili wa Mswada huu wameacha sehemu hii na kimsingi wakahamisha mzigo wa kulinda bei ya chai hadi ushuru unaolipwa na Wakenya.

Pia ina maana kwamba wakulima hawana tena hakikisho hazina ya kuthibiti bei ya chai itakuwa na fedha, kwani pesa hizo zitatolewa kupitia bajeti ya kitaifa na Bunge la Kitaifa.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO