Jamvi La SiasaMakala

Hata salamu za Mungu hamna kati ya Ruto na Gachagua

Na GEORGE MUNENE, BENSON MATHEKA November 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VITA baridi vya kisiasa kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua viliendelea hadharani jana wawili hao wakikosa kusalimiana walipokutana katika hafla ya kanisa kaunti ya Embu.

Wawili hao walihudhuria hafla ya kutawazwa kwa Askofu Peter Kimani Ndung’u wa dayosisi ya Kanisa Katoliki iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Embu.

Hii ilikuwa mara ya kwanza wawili hao kukutana tangu Bw Gachagua alipotimuliwa ofisini mwezi jana.

Katika hafla hiyo, Rais Ruto na Bw Gachagua hawakusalimiana, ikionyesha wazi tofauti zao za kisiasa zinaendelea.

Hata hivyo, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye alifika baada ya Rais Ruto alichangamkiwa na waumini na viongozi waliohudhuria.

Waumini waliojawa na furaha walimshangilia Bw Kenyatta kwa sauti kubwa alipokuwa na kutatiza sherehe hiyo kwa muda.

Ilibidi Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Anthony Muheria ambaye kuwakumbusha waumini kuwa walikuwa katika ibada ya Kanisa na walipaswa kunyamaza.

Bw Gachagua alifika mapema kabla ya Dkt Ruto na kuketi miongoni mwa waumini na kufuatilia sherehe

Hata hivyo Rais Ruto alipofika, Bw Gachagua hakusonga kukutana naye kumsalimia.

Wawili hao walikaa umbali mdogo kutoka kwa kila mmoja, lakini hawakupeana mikono hata kidogo.

Lakini Bw Kenyatta alikaa karibu na Prof Kindiki lakini hakushiriki mazungumzo naye au kiongozi wa nchi wakati wote wa hafla hiyo ambayo ilivutia mamia ya waumini, maaskofu na viongozi kote nchini.

Bw Kenyatta pia hakusalimiana na Bw Gachagua. Kabla ya kuondolewa mamlakani, Bw Gachagua aliashiria alikuwa amezika tofauti zake na Bw Kenyatta akisema alitumiwa kumshambulia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 na punde baada ya kuingia mamlakani.

Washirika wa Rais Ruto Gavana Cecily Mbarire, Seneta wa Embu, Alexander Mundigi, Mbunge wa Embu Kusini Nebart Muriuki, Mbunge wa Runyenjes, Eric Muchangi na Gitonga Mukunji wa Eneo Bunge la Manyatta walihudhuria.

Gavana Mbarire aliketi kando ya Dkt Ruto na wawili hao wakaendelea kuzungumza.

Hakuna kiongozi wa kisiasa aliyemtambua Bw Gachagua katika hafla hiyo isipokuwa viongozi wa kidini ambao walishangiliwa na umati walipotaja jina lake.

Gavana wa Embu Cecily Mbarire ambaye alikuwa mwenyeji, alimwalika Kindiki kuhutubia waumini, ambaye alimwalika Uhuru Kenyatta, kisha Kindiki akarudi jukwaani kumwalika Rais Ruto kukamilisha itifaki kabla ya hafla kukabidhiwa tena kwa Askofu wa Kanisa Katoliki. Peter Ndung’u.

Wakati wa hotuba zao, Bw Gachagua alikaa kimya akatazama maafisa wakuu wa serikali wakizungumza.

Muda mfupi baada ya hafla hiyo, Gachagua, akiandamana na washirika wake wa kisiasa Mlima Kenya akiwemo Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchoba waliondoka licha ya mwito wa baadhi ya waumini kumtaka ahutubu.

Baada ya kuondolewa mamlakani, Bw Gachagua alivuliwa wadhifa wa naibu kiongozi wa chama ambao ulikabidhiwa mrithi wake Kithure Kindiki ambaye alihudhuria hafla ya jana.

Haya yanajiri huku ikisemekana Bw Gachagua na Bw Uhuru wanasuka muungano kwa lengo la kupunguza ushawishi wa Rais Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Ruto alikuwa kwenye hafla hiyo lakini aliketi miongoni mwa waumini.

Rais Ruto aliwahakikishia Wakenya kuhusu kujitolea kwake kuhakikisha Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) inafanya kazi kwa manufaa ya Wakenya wote.

Mkuu wa Nchi alisema amepokea malalamishi ya Kanisa na Wakenya na akaahidi kusuluhisha matatizo ya SHIF yanayowakabili wananchi.

‘Makosa yaliyobainishwa na kanisa Katoliki katika SHIF yatarekebishwa, nataka kuhakikisha kuwa huduma za afya sio za matajiri. Utoaji wa afya kwa wote utaleta mabadiliko na hakuna Mkenya atakayeachwa nje,’ alisema Dkt Ruto.

Rais alisema Mtaala unaozingatia Mtaala (CBC) unafaulu na kuwataka Wakenya kuwa na subira na kuukumbatia.