Ruto alivyoyeyusha baraka za wahubiri na kupisha msimu wa lawama
KABLA ya kuingia mamlakani Septemba 2022, Rais William Ruto na kanisa walikuwa na uhusiano mwema.
Alihudhuria ibada katika kila kona ya nchi ambako alinukuu Biblia kwa urahisi, akivutia umati na hatimaye akaingia mamlakani.
Lakini uhusiano huu mzuri na Kanisa unafifia haraka, huku viongozi wa kidini wakigeuka kuwa wakosoaji wakali wa utawala wake wa Kenya Kwanza.
Mnamo Alhamisi, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) lilishutumu Rais Ruto kwa kuendeleza ‘utamaduni wa uwongo’ na kutumia vyombo vya serikali kuwanyamazisha wakosoaji.
“Utamaduni wa uwongo unachukua nafasi ya uadilifu na heshima ambayo Wakenya wanastahili. Kimsingi, inaonekana kwamba ukweli haupo, na kama upo, ni kile serikali inachosema,” alisema Mwenyekiti wa KCCB Askofu Mkuu Maurice Muhatia.
Hivi majuzi, taswira ya Mchungaji Dorcas Rigathi akiwa ameshikilia mkono wa mumewe Rigathi Gachagua na kuangua kilio walipokuwa wakitoka Hospitali ya Karen iliatua moyo watu wengi – hata wale ambao kwa kawaida hawakuwa wakikubaliana na siasa za Naibu Rais aliyetimuliwa.
Ilikuwa wakati huohuo ambapo Mwinjilisti Teresia Wairimu wa kanisa la Faith Evangelistic Ministries alipoteza utulivu wake wa kawaida na kukosoa utawala wa Ruto. “Siku zote nimekuwa nikifikiri kwamba serikali hii ni serikali ya Mungu; ni serikali ya vita,” alisema. Alionya kuwa huenda asimpigie kura Dkt Ruto 2027.
Dkt Ruto na Gachagua walipoapishwa katika uwanja wa kimataifa wa Moi mnamo Septemba 13, 2022, Wairimu alikuwa mmoja wa walioombea serikali mpya.
Hapo awali, alikuwa miongoni mwa viongozi wa kidini ambao walikuwa wamezunguka nchi nzima wakimpigia debe Ruto kama ‘ mgombeaji aliyetumwa na Mungu’ kinyume na Raila Odinga wa Azimio, ambaye alisawiriwa kama mtu ambaye njia zake hazikuwa za kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Baada ya ushindi wa Kenya Kwanza, Wairimu alimsifu Ruto, huku akimfananisha na Daudi katika Biblia, ambaye aliinuka kutoka kuchunga kondoo hadi kuwa mmoja wa wafalme wakuu wa Israeli.
Hata hivyo, kauli zake za kukosoa serikali zinaashiria mwisho wa ndoa iliyokuwa kati ya Kanisa na utawala wa Kenya Kwanza kwa ujumla na hasa Dkt Ruto.
Wairimu amekuwa kiongozi wa kiroho wa Rais Ruto na Mkewe Rachel. Katika ulimwengu wa kiroho, wawili hao ni watoto wake na kwa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya Rais, tunaweza kutumia maneno ya kisheria kusema anawanyima urithi wao wawili.
“Wakati Nabii halisi kama Teresia anaposema ‘baadhi ya watu wataanza kurudi nyumbani’, unabaki kuwazia maana ya usemi huo zaidi. Yeye hufungua kinywa chake na misimu hubadilika!
Ni wazi kuwa ni enzi mpya katika nchi hii na hali haitakuwa kama kawaida,” anasema Lilian Mandu, mkufunzi wa maisha.
Padri wa All Saints Cathedral la Kanisa Kianglikana nchini, Evans Omollo, aliwatahadharisha viongozi wenzake wa kanisa kujizuia kuidhinisha viongozi wa kisiasa kama “walioteuliwa na Mungu”, kutokana na ushawishi katika jamii
. Canon Omollo alishauri kwamba, katika siku zijazo, kanisa linapaswa kuwa mbali na masuala ya kisiasa,
Kasisi Tony Kiama wa Kanisa la River of God ni mmoja wa makasisi ambao wamekuwa wakipinga kile wanachotaja kuwa utovu wa nidhamu wa utawala wa Ruto.
Hivi majuzi alisema kwa uwazi kwamba utawala wa Kenya Kwanza haukuwa ukitumikia kusudi la Mungu. Mahubiri hayo yalikitwa katika Yohana 10:10 inayosema: “Mwizi haji ila kuiba na kuua na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”
Kasisi Kiama kisha alitoa mfano wa mauaji wakati wa maandamano ya Gen Z, kupanda kwa gharama ya maisha na ufisadi kama baadhi ya maovu ya Kenya Kwanza.
Katika mahojiano na gazeti la Taifa Jumapili, Kiama alisisitiza kwamba serikali hii ilidharau mamilioni ya Wakenya ambao walitarajia huduma.
“Lazima niwe wazi sana. Ninaposema serikali imefeli Wakenya namaanisha wote wawili Ruto na Gachagua na wanabeba lawama sawa kwa fujo tunazozipata. Walichaguliwa kwa pamoja, na sioni jinsi mmoja wao anavyoweza kugeuka na kudai kuwa walikuwa. hawawajibiki,” anasema.
Mkuu wa Christ is the Answer Ministers (Citam), Askofu Calisto Odede, anasema kwamba viongozi viongozi kidini hawakosei kuwakosoa viongozi wa kisiasa wanaposhindwa kutimiza wajibu wao.
“Ingawa Katiba inatenganisha serikali na dini, katiba pia inamtambua Mungu Muumba Mkuu. Kwa hivyo, hii inamaanisha kwamba kanisa haliwezi kujiondoa kabisa kutoka kwa masuala yanayohusu utawala wa watu wa Kenya kwa sababu tuko katika meli moja.
Kwa hivyo, hii ina maana kwamba tunapaswa kuwawajibisha wale ambao wamekabidhiwa uongozi wa taifa ili sote tuwe salama,” aliambia Taifa Jumapili.
Kasisi Edward Munene anasema amekuwa akianika kufeli kwa uongozi wa Kenya Kwanza. Katika mahojiano kwa njia ya simu, Kasisi Munene alisema kuwa kuna wengi kama yeye ambao wametamaushwa na uongozi wa nchi.
Mzozo unaoshuhudiwa kati ya Rais Ruto na viongozi wa kanisa unaibua suala la kuidhinishwa kwa wagombea urais na viongozi wa kidini na iwapo kuna manufaa au ni hasara kwa kanisa na taifa.
Kasisi Kiama anasema kuwa viongozi wa makanisa hawana biashara ya kuwaidhinisha wagombeaji wa viti vya kisiasa akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunawatenga baadhi ya waumini wa kanisa hilo ambao wanaweza kumuunga mkono mgombeaji tofauti.
Aidha anapuuza dhana maarufu miongoni mwa Wakristo hasa wa Kipentekoste kwamba Kenya ilikuwa taifa lililochaguliwa na Mungu.