Yafichuka wafanyakazi 6000 wa jiji hawajaenda likizo miaka sita wasikose marupurupu
SERIKALI ya Kaunti ya Jiji la Nairobi ilitumia jumla ya Sh18 bilioni katika mwaka uliopita wa kifedha kuwalipa wafanyikazi, huku takriban 6,000 kati yao wakikataa kwenda likizo zao za kila mwaka ili kuepuka kupoteza marupurupu.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Jiji la Nairobi Peter Imwatok Alhamisi alisema kwamba serikali ya kaunti haiwezi kutimiza majukumu yake ya maendeleo kutokana na zigo kubwa la mishahara ambalo limetishia kuilemaza.
Bw Imwatok aliwasilisha hoja ambayo sasa itawataka wafanyakazi wote ambao hawajaenda likizo ya mwaka kwa kipindi cha miaka minne hadi sita kutumwa kwa likizo ya lazima ili kudhibiti ongezeko la mishahara.
Madiwani waliambiwa kuwa baadhi ya wakurugenzi wakuu katika serikali ya kaunti na bunge la kaunti hawajaenda likizo yoyote kwa miaka sita iliyopita na hawataki kulipwa fidia kwa siku zao za likizo.
Baadhi yao pia ni wafanyikazi hewa, kulingana na maafisa katika serikali ya kaunti. “Tunapokea pesa kutoka kwa Mdhibiti wa Bajeti kila wiki lakini fedha hizo hazitoshi kuendesha serikali ya kaunti. Kila wiki, Waziri wa fedha hukopa pesa kulipa mishahara na marupurupu kwa maafisa. Hili lazima lifikie mwisho. Tunalea ufisadi kwa sababu baadhi ya viongozi hawa wanaogopa kukosa dili wakiwa likizo. Hatuwezi kufanya kazi hivyo,” Bw Imwatok alisema.
Hoja hiyo pia inalenga kuweka bayana kwamba wafanyikazi wote wa serikali ya kaunti ambao wametimiza umri wa miaka 60 wanapaswa kustaafu na kuzimwa kuongezwa kwa muda wao kazini.
“Wale ambao wamefikisha umri wa miaka 60 wanapaswa kuondoka madarakani na kumwachia mtu mwingine. Tunao vijana wa kujifunza kutoka kwao. Sheria inahitaji kwamba mara tu unapofikisha umri wa miaka 60, uende likizo ya kustaafu. Hatutaruhusu ukiukaji wa sheria kumfurahisha yeyote,” Bw Imwatok aliongeza.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA