Habari za Kitaifa

Tumefanya makosa lakini tutarekebisha, Ruto sasa awaambia maaskofu waliomkosoa

Na BENSON MATHEKA November 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto sasa ameungama kwamba kwamba serikali yake imetenda makosa mbalimbali na kuahidi kuyarekebisha.

Dkt Ruto ameonekana kubadili msimamo siku moja tu baada ya kuwakashifu maaskofu wa Kanisa Katoliki waliotaja maovu kadhaa yanayotekelezwa na utawala wake akiwaonya dhidi ya kueneza kauli zisizo za ukweli “kuhusiana na masuala mahimu yanayohusu masilahi ya umma.”

Maaskofu hao, chini ya mwavuli wa Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki (KCCB), Alhamisi waliukashifu utawala wa Rais Ruto kwa kuendeleza “mwenendo wa kutoa kauli za uwongo” na kufeli kutimiza ahadi muhimu ilizotoa kwa Wakenya.

Lakini akizungumzia suala hilo Jumamosi wakati wa kutawazwa kwa Askofu Peter Kimani Ndung’u kuwa Askofu wa Kanisa Katoliki, Dayosisi ya Embu, Rais Ruto alikoma kuwashutu viongozi hao.

Alitambua masuala yaliyoibuliwa na maaskofu hao na kuahidi kushughulikia mapungufu ya serikali inapowahudumia raia.

“Nawashukuru maaskofu wetu kwa kutuambia kuwa kuna makosa hapa na pale. Kwa hivyo, ningependa kuwahakikia pamoja na Wakenya kuwa tutayarekebisha ili nchi yetu isonge mbele,” Dkt Ruto akasema wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Embu, kaunti ya Embu.

Rais pia aliahidi kuhakikisha kuwa mipango ya serikali yake kama vile Mpango wa Afya Kwa Wote (UHC), mpango wa Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu (AHP) inafanikiwa kwa manufaa ya Wakenya.

Mnamo Ijumaa, Novemba 15, 2024, Dkt Ruto, akihutubu wakati wa sherehe ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Tangaza, Nairobi, aliwaonya maaskofu wa Kanisa Katoliki dhidi ya kueneza habari zisizo sahihi kuhusu utendakazi wa serikali yake “kwani zitawarudia baadaye.”

“Nataka kuomba sote, viongozi, maaskofu na Wakenya, tushirikiane ili tujenga taifa ambalo tutafurahia. Hata tunapotoa kauli kuhusu masuala yenye umuhimu kwa Wakenya, tuhakikishe ni za kweli ili tusije tukawa waathiriwa wa yale tunawashutumu wengine kutenda. Najua mwafahamu ninachomaanisha,” akaeleza.

Mnamo Alhamisi Novemba 14, 2024 maaskofu hao wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza la KCCB Maurice Muhatia pia waliisuta serikali kwa kuendeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu kama vile uketaji nyara wakosoaji wake.