Akili MaliMakala

Chuo chaanzisha utengenezaji wa divai ya zambarau

Na SAMMY WAWERU November 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ZAMBARAU ni aina ya tunda linalojikuza mwituni, hasa kandokando mwa mito.

Kiingereza, linajulikana kama Jamun, na ni beri ya rangi ya zambarau au nyeusi inayokua kwenye mti wa Syzygium cumini.

Ni wakulima wachache mno wanaotambua thamani yake, wanaokuza mizambarau.

Tharaka Nithi ni mojawapo ya maeneo yanayolima zambarau, na Chuo Kikuu cha Chuka kilichoko katika kaunti hiyo kipo kwenye mtandao huo.

Nembo ya divai ya zambarau. PICHA|SAMMY WAWERU

Huku wengi wakikosa kutambua thamani yake, chuo hicho kinaongeza thamani matunda hayo ili kuvutia wateja.

“Matunda ya zambarau, aghalabu, yanapatikana katika nchi za tropiki na si watu wengi wanajua tija zake,” anasema Whitney Nyambura, mwanafunzi wa mwaka wa nne Chuo Kikuu cha Chuka.

Yana faida kadha wa kadha kiafya, ambapo yamesheheni virutubisho vya Vitamini C, madini ya Iron – yanayosaida kuongeza kinga mwilini, ikiwa ni pamoja na antioxidants.

Hali kadhalika, zambarau ina madini yanayosaidia kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, hivyo ni bora kwa wagonjwa wa maradhi ya Kisukari, pasi kusahau kulainisha ngozi, na kuwa na Potassium.

Whitney Nyambura, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Chuka akionyesha divai ya matunda ya zambarau. PICHA|SAMMY WAWERU

Nyambura, ambaye anasomea Digrii ya Masuala ya Sayansi ya Chakula na Teknolojia, anadokeza kwamba zambarau ikiongezwa thamani inateka soko lenye ushindani mkuu.

“Matunda ya zambarau mara nyingi huharibikia mitini ilhali yanaweza kugeuzwa bidhaa yenye thamani,” Nyambura anasema.

Chuo Kikuu cha Chuka kupitia kitengo chake cha Sayansi ya Chakula na Teknolojia huunda divai.

Kileo cha zambarau, kilikuwa kati ya bidhaa zilionyeshwa wakati wa Kongamano la Mtandao wa Kitaifa unaoleta pamoja washirika wa Kilimo kutoka Sekta ya Umma na Kibinafsi, ndio ASNET, mwaka huu, 2024.

Divai ya ndizi (kushoto) na ya zambarau, zilizoundwa na Chuo Kikuu cha Chuka. PICHA|SAMMY WAWERU

Kongamano hilo lilifanyika kati Oktoba 1 na 2.

“Matunda kama zambarau hayatiliwi maanani ilhali yana manufaa chungu nzima kiafya. Yakisindikwa kuwa divai, kipimo cha mililita 750 kitauzwa kuanzia Sh2, 000,” Nyambura akaambia Akilimali Dijitali wakati wa kongamano la ASNET lililofanyika KICC, Nairobi.

Waziri wa Kilimo, Dkt Andrew Karanja ndiye alifungua rasmi hafla hiyo na alisisitiza kuhusu mtandao wa uchakataji bidhaa za kilimo.

“Uongezaji thamani unateka soko bora, si tu hapa nchini ila katika masoko ya ng’ambo na serikali iko tayari kushirikiana na wadau husika kufanikisha mtandao huo,” Dkt Karanja akasema.

Whitney Nyambura, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Chuka akielezea kuhusu divai ya ndizi. PICHA|SAMMY WAWERU

Chuo Kikuu cha Chuka, hata hivyo, kinaendelea kushughulikia kibali kutoka kwa Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) kuingiza divai ya zambarau sokoni.

Taratibu za uundaji wa kileo hicho ni sawa na zile za kuandaa pombe, zinazojumuisha uchachu.

Bidhaa zinazohitajika, kando na zambarau ni pamoja na chachu, maji na sukari, Nyambura akielezea kwamba huchukua muda wa mwezi mmoja divai kuwa tayari.

Kando na divai, Chuo Kikuu cha Chuka pia kinaunda vitafunwa kwa kutumia nafaka. PICHA|SAMMY WAWERU

Mbali na divai ya zambarau, mwanafunzi huyo pia amebobea kutengeneza kileo cha ndizi.

Uongezaji thamani bidhaa za kilimo kunatajwa kama njia mojawapo kuokoa mazao mabichi ya kilimo, hasa msimu wa mvua na soko linapokosekana.