Zaidi ya waumini 1,000 wafika mazishi ya ‘Nabii’ Akatsa wengi wakimsifu kuwasaidia kupata ajira
MWAZILISHI wa Kanisa la Jerusalem of Christ Church Nabii Dorcus Mary Sinaida Akatsa alizikwa Jumamosi mtaani Kawangware.
Waumini zaidi ya 1,000 walimininika nyumbani kwake kutoa heshima za mwisho.
Baadhi ya waumini ni wale ambao walimmiminia sifa kwa kuwawezesha kupata nafasi katika vitengo mbalimbali vya usalama nchini pamoja na marubani.
Bw Samuel Kobe, ni miongoni mwa wanajeshi ambao walihudhuria ibada ya mwisho ya nabii huyo.
Bw Kobe alisema baada ya kupatana na nabii huyo akifanya usherati na kuwa mlevi alimwombea na kumuunganisha na kikosi cha polisi.
“Nikiwa hapa Kawangware, mami (Akatsa) aliniombea hadi nikapata kujiunga na kikosi cha polisi. Wakati nilimaliza nilitumwa eneo lenye ukame. Nilirudi hapa kumweleza na akanipikia chapati 300 niende nazo,” alihuzumika Bw Kobe.
Bw Kobe aliambia umati kuwa maombi ya nabii huyo pia yalimwezesha kupandishwa vyeo mbalimbali.
“Kila wakati aliniombea nilipata kupandishwa vyeo. Kama ni kuzuru mataifa nimezuru zaidi ya 20,” aliongeza.
Akasta alipata heshima ya mwisho kutoka kwa waumini wake na wanasiasa mbalimbali ambao walihudhuria.
Kulingana na viongozi wa kisiasa ambao walihudhuria mazishi ya nabii huyo walisema uamuzi wa kuzikwa katika mtaa wa Kawangware ni kulinda shamba hilo ambalo pia lilikuwa likimezewa mate na watu fulani.
Wakili wa familia hiyo ambaye ni Seneta wa Nairobi Bw Edwin Sifuna alisema atazidi kuungana na wana wa Akasta (David Jogoo na Moses Sangolo) kuhakikisha mali yake hainyakuliwi.
Bw Sifuna alidokeza kuwa alikutana na nabii huyo kabla ya kuchanguliwa kuwa seneta wa Nairobi.
“Alinitembelea kwenye afisi yangu akaniombea na kunielezea matatizo yake. Alihakikisha tiketi yangu ya ndege ya kusafiri kutoka Nairobi hadi Kakamega inapatika kila wakati. Hadi pale nilifanikiwa kuweka mambo sawa,” alisema Bw Sifuna.
Hata hivyo, kuna wale ambao walimwandama nabii huyo baada ya uchanguzi 2022. Wanyakuzi wakitaka pia kuchukua mali Akatsa.
Bw Sifuna alisema kabla ya kufariki kwa nabii huyo walielekea mahakamani mara mbili na nabii huyo ambaye alimuomba akabidhii faili hiyo kwa mwanawe mdogo.
“Aliniita siku hiyo na kunieleza kuwa nimekuwa mdosi nikabidhi faili kwa kijana mdogo. Aliniambia niweze kuangalia kesi hiyo kutoka juu na kwa sababu ya hiyo heshima, mimi nataka niwahakikishie kwamba hakuna siku kutatokea jambo na Sifuna asipatikane kwa ajili ya kusimama na hii kanisa na kusimama na familia ya mami na kulinda viwanja vyake vyote ambavyo Mungu alikuwa amembariki navyo,” alisisitiza Bw Sifuna.
Kiongozi huyo aliwataka waumini kutafuta kiongozi mwingine ambaye atavalia kiatu cha nabii huyo ili kuunganisha waumini hao.
“Mungu amechukua yule amekuwa akifikisha dua zetu za maombi kwa Mungu. Hivi sasa tunaomba Mungu atupee nabii mwingine,” alikamilisha Bw Sifuna.
Aliyekuwa mwakilishi wa Wadi ya Gatina, Bw David Ayoi alisema kuwa awali kulikuwa na walaghai ambao walitaka kumnyang’anya nabii huyo ardhi ya Kawangware 56 ambayo alijenga kanisa la Jerusalem of Christ Church.
Kiongozi huyo alisistiza kuwa mwili wa nabii huyo kuzikwa katika eneo hilo kutapunguzia tamaa kwa wale wanaotaka kuiiba.
“Mama aliniita baada ya shamba lake kupangiwa na walaghai na hivyo nikamtafutia Seneta Sifuna. Kuzikwa hapa Kawangware ni kulinda shamba hili,” alisistiza Bw Ayoi.