MLIMA UMEENDA? Dalili zajitokeza kwamba Mt Kenya ni telezi kwa Rais Ruto
RAIS William Ruto sasa anakabiliwa na wakati mgumu kisiasa katika eneo la Mlima Kenya baada ya kuzomewa na kupata mapokezi baridi kwenye hafla ya kutawazwa kwa Askofu wa Dayosisi ya Embu Peter Kimani mnamo Jumamosi.
Hafla hiyo ambayo iliandaliwa katika Chuo Kikuu cha Embu ilihudhuriwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua miongoni mwa wanasiasa wengine kutoka Mlima Kenya.
Ingawa ilikuwa hafla ya kidini ambayo siasa hazikupigwa, kilichojitokeza ni kuwa Rais alizomewa na ni dhahiri amepoteza uungwaji mkono wa eneo hilo huku Bw Gachagua na Bw Kenyatta wakionekana kuvuna pakubwa mlimani.
Alipowasili, Rais Kenyatta alishangiliwa na umati tukio ambalo halingefanyika kuelekea uchaguzi wa mnamo 2022 wakati alipokuwa akiunga mkono Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Bw Kenyatta aliposimama kuhutubu baada ya kualikwa na Profesa Kindiki alishangiliwa na umati na wakati wa hotuba yake alionekana kuchangamsha wananchi mno.
Sina stori nyingi
“Mimi sina mengi ya kusema mimi siku hizi sina stori nyingi. Mimi huangalia tu televisheni na kusikiza redio. Tuombee nchi yetu, amani na uwiano na wananchi kisha tuache mambo ya ukabila na tupendane,” akasema Rais Kenyatta huku akishangiliwa na wananchi katika kila tamko lake.
Baada ya hafla hiyo kukamilika, Bw Kenyatta aliondoka kuelekea kwenye gari lake lakini vijana wengi wakamfuata huku wakimshangilia. Hii ilikuwa ishara kuwa huenda wamemkumbatia na ‘kujutia’ hatua yao ya kuunga utawala wa sasa jinsi alivyowaonya kuelekea kura ya 2022.
Hali ilikuwa hiyo hiyo kwa Bw Gachagua ambaye alilakiwa kishujaa na umati uliomsindikiza hadi hema alimoketi mkabala wa Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba na mwenzake wa Maragua Mary Wamaua.
Ingawa hakupewa muda wa kuhutubu, kila mara jina la Bw Gachagua lilipotajwa, umati ulipiga kelele na kumshabikia. Sherehe ilipokamilika, vijana walimwandama wakiimba ‘Riggy G’ na wakamsindikiza hadi kwenye gari lake huku baadhi wakisema wazi ndiye kiongozi wao wa Mlima Kenya.
Kwa upande mwingine, Rais Ruto hakuchangamkiwa, alizomewa, hotuba yake ilionekana kuwa vuguvugu na kukosa mnato na ilikuwa wazi hata Profesa Kindiki licha ya kutoka eneo hilo la Mlima Kenya Mashariki pia raia hawakuwa na shughuli naye.
Kwa kipindi kimoja wakati wa hotuba yake, Rais Ruto alizomewa na umati ambao walikuwa wakikataa baadhi ya hoja alizokuwa akifafanua kuhusu sekta ya elimu, afya na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Mapokezi waliyopata Uhuru na Rigathi
Mapokezi waliyoyapata Rais Kenyatta na Bw Gachagua yalionyesha kuwa wanasiasa hao wawili ndio huenda wakaamua mustakabali wa eneo la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi wa mnamo 2022.
Bw Gachagua ambaye alitimuliwa kupitia hoja iliyowasilishwa bungeni, bado anapambana mahakamani kwenye kesi anayoomba asitimuliwe mamlakani.
Kwa mujibu wa katiba, iwapo Bw Gachagua atapoteza kesi hiyo ambayo ina uwezekano wa kufika hadi Mahakama ya Juu, basi atakuwa kwenye kijibaridi kisiasa kwa muda wa miaka 10.
Mbunge wa Saboti Caleb Amisi alisema kuwa ni wazi kuwa eneo la Mlima Kenya halina haja na utawala wa Rais Ruto tena.
Wengi wa wachanganuzi wa kisiasa wamehusisha masaibu ya Bw Gachagua na ahadi za uongo kama zilizodidimiza umaarufu aliokuwa nao Rais Ruto Mlima Kenya.
“Eneo la Kati limeenda kabisa ama kabisa limeenda,” akaandika Bw Amisi kwenye ukurasa wake wa X.
Kati ya kura milioni 7.1 ambazo Rais Ruto alizoa na kushinda urais mnamo 2022, karibu milioni nne zilitoka kaunti ambazo zilipatikana ukanda wa Mlima Kenya.
Kwa mujibu wa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha USIU Profesa Macharia Munene, Rais Ruto hana lake mlimani na maeneo mengine ya nchi “kutokana na uongo ambao hauishi kwenye kinywa chake”.
Chuki na kupigwa vita
“Mlima Kenya hoja hata is Gachagua bali chuki na vita alivyopigwa kutokana na baraka za Ruto na ni jambo lisilowezekana apate uungwaji mkono eneo hilo tena. Wakazi wako tayari kulipiza kisasi kutokana na Bw Gachagua kutotendewa haki na ahadi ambazo Rais anatoa na hazitimizi,” akasema Profesa Macharia.
“Raila ni mwanasiasa ambaye hatagemewi na akiona umaarufu wa Ruto haupo, hatamuunga mkono. Dalili za Rais kupoteza mlimani zilianza zamani na kilichotokea Embu kinamwonyesha kuwa sasa aanze kujipanga na maeneo mengine,” akaongeza.
Wakili na mwanasiasa mbishi Miguna Miguna naye alienda mitandaoni na kusema Rais Ruto hawezi kushinda kura za 2027 wala asitegemee kuwa ataungwa mkono na ngome za Raila baada ya kupoteza Mlima Kenya.
“Mtu asikudanganye kuwa Waluo na Waluhya watamwokoa. Eneo la Nyanza haliwezi kumuunga William Ruto wala asitegemee hilo,” akaandika Bw Miguna kwenye mtandao wake wa X.