Habari za Kitaifa

Mbadi: Nimegundua kuna shida kubwa na ugavi wa pesa; nishaongea na Rais

Na GEORGE ODIWUOR  November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Fedha John Mbadi amependekeza mageuzi yafanywe kuhusu namna fedha za maendeleo zinagawanywa kutoka serikali ya kitaifa hadi maeneo mbalimbali nchini.

Alisema baada ya kuteuliwa kuwa katika wadhifa huo, aligundua kuna dosari nyingi kuhusu namna pesa hutumwa kutoka serikali kuu hadi mashinani kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Bw Mbadi alisema dosari katika usambazaji wa fedha za maendeleo kwa maeneo mbalimbali zinachangia utovu wa usawa kimaendeleo nchini.

“Nimezungumza na Rais William Ruto na kumshauri kuwa usawa unafaa kuzingatiwa wakati wa usambazaji wa pesa kwa maeneo kadhaa nchini,” akasema.

Kulingana na Bw Mbadi kuna maeneo nchini ambayo hupokea fedha nyingi kuliko maeneo mengine ilhali maeneo yote yanapasa kugawiwa kiasi sawa cha pesa za maendeleo.

Akiongea alipokutana na wakazi wa Kibura, eneo bunge la Suba Kusini, Kaunti ya Homa Bay, waziri huyo alisema kuwa miradi kadhaa imekwama katika maeneo mbalimbali kwa kunyimwa fedha bila sababu.

Bw Mbadi aliahidi kurekebisho makosa kama hayo yaliyotekelezwa na maafisa wa serikali ambao ni watundu.

Alisema, kwa mfano, maeneo ya Kaskazini Mashariki hupokea fedha finyu za maendeleo ikilinganishwa na maeneo mengine eneo hilo linapasa kuinuliwa kwa sababu imesalia nyuma kimaendeleo tangu uhuru.

Akitoa mfano kuhusu miradi ya ujenzi wa barabara, Bw Mbadi alisema kuwa kuna eneo lililotengewa Sh151 bilioni kwa miradi ya barabara inayoendelea kutekelezwa.

“Aidha, utapata eneo fulani ikitengeza Sh81 bilioni na lingine ikitengewa Sh77 bilioni. Lakini kaunti kama Samburu itatengewa Sh77 milioni za miradi ya barabara,” Bw Mbadi akasema.

Kulingana na Waziri huyo wa Fedha, kaunti kama Homa Bay ilitengewa Sh12 milioni za ujenzi wa barabara kabla ya kuteuliwa kwake huku Siaya na Migori zikitengewa pesa kidogo hata zaidi.

Bw Mbadi alisema anataka kutekeleza mabadiliko kuhusu namna fedha za maendeleo zinatengwa kwa maeneo mbalimbali kutoka serikali kuu.

“Mimi sio waziri wa jamii ya Waluo au eneo la Nyanza pekee. Mimi ni waziri wa Kenya yote na sharti nihakikishe ugavi sawa wa fedha za maendeleo kote nchini,” akasema.

Bw  Mbadi alisema maeneo yote nchini yanahitaji maendeleo kwa sababu Wakenya wote wanalipa ushuru.

Aliukosoa utawala uliopita wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika eneo la Kati mwa Kenya huku maeneo mengine yakitelekezwa.

Bw Mbadi aliapa kwamba chini ya hatamu yake kama Waziri wa Fedha atahakikisha kuwa maeneo yote yanapata ugavi sawa wa fedha za maendeleo.

“Vile vile, nitahakikisha kuwa miradi ya barabara iliyoanzishwa hapa Homa Bay haikwami bali inakamilishwa,” akasema.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mbita-Sindo-Magunga-Sori inayounganisha fuo za Ziwa Victoria zilizoko katika kaunti za Migori na Homa Bay.

Mradi huo ulianza miaka saba iliyopita.

Rais William Ruto alizindua upya mradi huo mnamo Oktoba 2023 lakini shughuli za ujenzi zimekuwa zikiendelea polepole zaidi.