Habari za Kitaifa

NTSA, kaunti kukarabati barabara zilizosheheni ajali msimu wa sherehe ukiwadia

Na VICTOR RABALLA November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAUNTI ya Kisumu imeanza mpango wa kukarabati barabara za maeneo ambayo ajali hutokea mara kwa mara ili kuzuia idadi ya vifo ambavyo vinaendelea kuongezeka.

Meneja wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi Barabani (NTSA) Isaac Silali amesema kuwa wametambua maeneo hayo hatari ambapo kaunti itakarabati barabara kwenye mzunguko wa Coptic na ile inayokutanisha barabara mbalimbali katikati mwa jiji hilo.

Hatua ya kukarabati barabara hizo imechukuliwa kutokana na mapendekezo ya Kamati ya Uchukuzi na Usalama kwenye Kaunti ya Kisumu (CTSC).

Bw Silali alisema hatua kubwa imepigwa katika kukarabati maeneo ambayo ajali ilikuwa ikitokea mara kwa mara katika barabara kuu ya Kisumu-Kakamega.

“Kwa ushirikiano na Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu Nchini (KENHA) tumeweka alama za barabarani, onyo, kujenga vizingiti vya kudhibiti kasi ya magari,” akasema Bw Silali.

Alikuwa akiongea wakati wa kuwakumbuka walioaga dunia na waliopata majeraha kutokana na ajali za barabarani jijini Kisumu.

Alisema kuwa asilimia 40 za ajali hutokea kutokana na magari yanayoendeshwa kwa kasi na wanalenga kudhibiti matukio hayo.

Aliwataka waendeshaji magari nao wawe makini na wasiyaendeshe magari wakiwa wamelewa huku akitaka abiria pia wamakinikie usalama wao.

Huku mwezi wa Disemba ambao huwa ni msimu wa sherehe ukinukia, NTSA inapanga kushirikiana na polisi kuimarisha usalama barabarani na kuwakamata wanaokiuka kanuni za trafiki.