Akili Mali

Anavyolisha mikahawa ya kifahari kwa uyoga

Na SAMMY WAWERU November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KARIBU miaka mitano iliyopita, Dennis Macharia aliamua kuingilia kilimo cha uyoga, biashara anayosisitiza kamwe hajutii kuikumbatia. 

Anasema hatua hiyo ilitokana na mahangaiko aliyopitia akikuza mboga.

Alikuwa mkulima wa mboga aina ya kabeji na dhania.

Wakati wa kutafutia mazao soko, Macharia anasema ilikuwa kibarua.

“Nilihangaishwa na mabroka sana,” akumbuka.

Vilevile, alikuwa mfugaji wa kuku, biashara nyingine anayolalamika aliisitisha kwa sababu ya mfumko wa bei ya chakula.

Chakula cha mifugo, hasa cha kuku, Covid-19 ilipotua Kenya 2020, bei iliongezeka mara dufu.

Dennis Macharia mkulima wa uyoga Githunguri, Kaunti ya Kiambu. PICHA|SAMMY WAWERU

Macharia hakufa moyo, na ni kupitia utafiti wa kina intaneti alipata wazo jingine.

Alitiwa motisha na mwekezaji na mkulima hodari wa uyoga Amerika, maarufu kama Paul Stamets.

“Kwenye mojawapo ya kitabu chake mitandaoni (e-book) kuhusu kilimo cha uyoga, nilishawishika ni biashara itakayotuliza moyo wangu,” anaelezea.

Kulingana na Macharia, maamuzi aliyofanya hakurejea nyuma tena.

“Licha ya changamoto nilizopitia wakati wa utangulizi, sikufa moyo,” anasema.

Kwa mtaji wa Sh20, 000 alianzisha kilimo cha uyoga, na sasa anajivunia kuwa mwasisi wa Garden Mushrooms, kampuni inayowika nchini katika ukuzaji wa zao hilo la familia ya Fungi.

Macharia ambaye pia anafanya kazi katika kampuni ya kuuza dawa, alianzisha ukuzaji wa uyoga akishirikiana na mkewe.

Kuelewa mtandao wa soko, hata hivyo, haikuwa rahisi.

“Tulipoanza, uyoga ulikuwa ukiuzwa katika mikahawa na hoteli za kifahari haswa eneo la Westlands, Nairobi,” anasema, akiongeza kuwa lengo lake lilikuwa kuona mwananchi wa mapato ya chini pia anapata tonge la uyoga.

‘Shamba’ la uyoga la Dennis Macharia Kiambu. Uyoga unasifiwa kusheheni virutubisho na madini anuwai. PICHA|SAMMY WAWERU

Uyoga unasifiwa kusheheni Vitamini D na B, Potassium, antioxidant, kuboresha ubongo na kufanya mifupa iwe imara.

Ukitajwa kama mojawapo ya kiini cha virutubisho vya Protini badala ya nyama, uyoga pia umesheheni fiber, kiwango chake cha calorie kikiwa cha chini, na vilevile hupunguza makali ya maradhi yanayohusishwa na afya, tija hizo zikiwa chache tu kuorodhesha.

Macharia anataja uyoga kama zao la hadhi, ambalo kando na kuwa na virutubisho anuwai kisiha, humuingizia mapato na kuinua jamii – kupitia ajira.

Aligeuza chumba kizee cha kuku kufanya upanzi wa uyoga, na sasa anajivunia kuwa na ‘mashamba’ matatu.

Ni majengo ya kisasa kulima uyoga, la kwanza likiwa la kipimo cha futi 60 kwa 20, la pili futi 70 kwa 10, na la tatu, futi 30 kwa 10.

Majengo ya uyoga ya Dennis Macharia, tayari kufanya upanzi wa zao hilo lenye soko mithili ya mahamri moto. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, yana mitambo ya kisasa kusawazisha hewa na pia yana kamera (CCTV) kufuatilia utendakazi.

Miaka mitano baadaye, Garden Mushrooms imekua kwa kasi; kutoka wafanyakazi wanne, hadi kumi wa kudumu, na wengine 15 wakiwa vibarua.

“Ni biashara inayotupa tabasamu, na tumeipalilia kwa kuirejeshea mapato,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano nyumbani kwake Matuguta, Githunguri, Kaunti ya Kiambu.

Macharia pia amewekeza kwenye vyumba vya kisasa vya baridi, kupitia ufadhili wa Kenya Climate Innovation Center (KCIC).

Soko, alidokeza kwamba hulenga mikahawa na hoteli za hadhi na kifahari Kiambu na Nairobi, maduka ya kijumla ndiyo supermarket, na vilvile ana wateja City Park, Nairobi.

Dennis Macharia na wafanyakazi wake wakifuatilia uyoga unavyoendelea kukua. PICHA|SAMMY WAWERU

Chumba kimoja, anabashiri huzalisha paneti 4, 500 za gramu 250 kwa msimu, bei ikichezea kati ya Sh180 hadi Sh200 kila kipakio.

Kuanzia maandalizi hadi mavuno, uyoga huchukua karibu siku 42.

Licha ya mafanikio, anataja kupata mbegu kama mojawapo ya changamoto anazopitia.

Mbegu za uyoga zinajulikana kama spawns, na hukuza aina ya white button mushrooms.

Huzitoa Afrika Kusini au Holland, gharama anayosema ni ya juu mno.