Habari za Kitaifa

Tutawaongoza Wakenya kukaidi kulipa ushuru, viongozi wa kidini waonya serikali

Na VICTOR RABALLA November 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa kidini kutoka Nyanza sasa wametishia kuongoza umma kuasi serikali ikiwemo kukataa kulipa ushuru, ili kulalamikia wanachotaja kama ukandamizaji unaozidi kuongezeka na usimamizi mbaya chini ya serikali ya Kenya Kwanza.

Viongozi hao kutoka kanisa la Kianglikana Kenya (ACK) na Baraza la Makanisa Nchini (NCCK) wameishutumu serikali kwa ukandamizaji na “kugeuza uongozi wa kisiasa kuwa biashara” kupitia kubuni serikali jumuishi.

Huku sauti za upinzani zikisalia kimya katika eneo la Nyanza, Askofu wa ACK Bondo David Kodia, amemshutumu Rais William Ruto kwa kuendeleza uongozi wa unyanyasaji, usimamizi mbaya kiuchumi na kuhujumu kanuni za taifa kuhusu demokrasia.

“Kukataa kulipa ushuru kutakosesha mihimili yote ya serikali fedha inazotumia kuwaingiza baridi Wakenya na ndio mbinu murwa,” alisema Askofu Kodia.

“Wakenya wanahitaji kuheshimiwa sio kutishiwa na kuadhibiwa kwa maoni yao tofauti,” alisema katika hotuba ya pamoja iliyotolewa katika kanisa la ACK St Stephens Cathedral, Kisumu.

Wakinukuu Mithali 29:2, viongozi hao walionya dhidi ya “utawala mbovu,” waliosema umewaacha Wakenya wakitaabika chini ya mzigo mzito wa ushuru, huduma za umma kuzorota na ukandamizaji kisiasa.

Viongozi hao wa kidini waliapa kutoa sauti mbadala inayoweza kuangazia serikali, wakisema serikali jumuishi inadhamiriwa kunufaisha tabaka la juu la kisiasa huku Wakenya wa kawaida wakizidi kuteseka.

“Hii leo hakuna kiongozi hata mmoja wa kisiasa kutoka eneo hili aliye na ujasiri wa kuangazia ukiukaji wa haki unaoendelea. Wote wamestarehe kwa sababu yote yanaonekana kumwendea shwari kiongozi wa ODM Raila Odinga.”

Askofu wa ACK Dayosisi ya Nyanza Kusini, Simon Onyango, alitaja ufurushaji wa aliyekuwa naibu rais, Rigathi Gachagua kama, “mwanzo wa mapinduzi mapya.”

“Kenya imeishia kuwa utawala wa kiimla wa chama kimoja pasipo kipimo kwa mamlaka ya rais kwa kila Mkenya aliye hai na yule bado hajazaliwa.”

“Bado hatujaona utekelezaji wa vitu alivyoahidi Rais wakati wa maandamamo mafupi ya Gen Z. Uzoroteshaji huu wa kaunti zetu ni sharti upingwe,” alisema.

Alimtaka rais kutangaza hadharani kuhusu hali ya afisi za Mama Taifa na Mke wa Naibu Rais baada ya kuahidi zitavunjiliwa mbali kwa sababu zinakiuka katiba.

Askofu wa ACK Maseno Kusini, Charles Onginjo, vilevile aliikashifu idara ya mahakama kwa kuwa mstari wa mbele kukandamiza haki za raia na kuegemea upande wa utawala wa “unyanyasaji.”

“Korti hazijakuwa na ujasiri wa kutangaza msimamo wao kuhusu utekaji nyara na mauaji kiholela ya raia wasio na hatia,” alisema.

“Badala yake, jaji mkuu huonekana na anapenda kuwa kando ya serikali kila fursa inapojitokeza.”

Askofu wa Church of Christ in Africa Patrick Ligawa, pia aliitisha mikataba ya sasa ya ajira na majukumu ya kifedha kwa wafanyakazi wa ikulu ikiwemo waombezi wanaolipwa.

Kuhusu mgomo wa wahadhiri unaoendelea, Askofu wa Free Pentecostal Church of Kenya Bishop Clement Otieno, alihimiza serikali kutekeleza mara moja mkataba wa malipo (CBA) ili kuruhusu utulivu kurejea katika taasisi za elimu ya juu.