TAHARIRI: Ukosoaji ndio husaidia serikali kujiimarisha
IPO kauli moja isemayo kwamba bora mtu kuwa na wakosoaji badala ya kuwa na rafiki nafiki.
Rafiki nafiki ndiye adui mkubwa wa mtu kwa sababu yeye hukubaliana nawe kwa kila usemalo na ufanyalo.
Katika mantiki hii basi, rafiki wa namna hii ni adui kwa msingi kwamba hakuongezei thamani yoyote.
Kwa upande wa pili, mkosoaji ni mtu wa maana sana. Ila ni vyema katika hatua hii ibainishwe kwamba si lazima mkosoaji awe adui. Hata kwa kweli maadui wa mtu hawawi wakosoaji wake! Adui ataafadhalisha kunyamaza ili ufeli ndipo afumbue kinywa kuzungumzia jinsi alijua kwamba ungefeli.
Manufaa ya mkosoaji ni kwamba huwezesha anayekosolewa kujua mapungufu yake. Iwapo mwenye kukosolewa ni mtu mwenye busara, basi atajirekebisha na kuchukua mkondo sahihi na mwishowe kuwa kipenzi cha watu anaowatumikia.
Inawezekana pia kwamba katika hali ambapo mwenye kukosolewa ni mtu mwenye busara, ataishia kuwa rafiki ya yule aliyemkosoa kwani ukosoaji huo utakuwa umechangia katika mabadiliko yaliyoishia kumfaidi mlengwa.
Ni kwa kuzingatia falsafa hii ambapo mifumo mashuhuri ya demokrasia duniani uwe ni uongozi unaozingatia mfumo wa Bunge au Urais, huwa kuna nafasi ya upinzani.
Upinzani katika taifa lolote lile ni asasi muhimu kwa demokrasia ya taifa. Hii ni kwa sababu, mbali na uongozi wa nchi kuwa na mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama, mrengo wa kisiasa wa Upinzani husaidia kuwa macho ya umma kwa kuanika maovu na makosa ya serikali tawala.
Hii ndiyo sababu katika mataifa mengi kiongozi wa upinzani ni mtu muhimu sana. Huwa na ofisi na wafanyakazi ambao wanalipwa mishahara kutoka kwa mfuko wa mlipa ushuru. Waasisi wa mifumo ya uongozi wa kisiasa walifahamu umuhimu wa jukumu la upinzani ndiyo sababu kukawepo mpangilio huo.
Tukirejelea nchi yetu na hasa matukio ya hivi karibuni, asasi ya dini ni asasi nyingine muhimu sana katika jamii. Dini tangu jadi ni chemchemi ya maadili. Jukumu la msingi la dini ni kuelekeza waumini na kuwapa lishe ya kiroho ili wawe watu wema na kuishi maisha ambayo yanapendeza machoni pa Muumba pamoja na binadamu wenzao.
Viongozi wa dini katika muktadha huu, wana jukumu la kuelekeza na hata kukosoa serikali itokeapo kwamba itapotea njia. Viongozi hawa watekelezapo jukumu hili, viongozi wa serikali wanafaa kuketi na kujisaili nafsini. Hii ni kwa sababu viongozi wa dini si wanasiasa na hawafai kuwa na miegemeo ya kisiasa.
Serikali inafaa kuwasikiliza viongozi wa dini kisha kufanya marekebisho kwa maslahi ya raia.