Ndio, ni kubaya lakini Kenya Kwanza itafaulu na kunyamazisha wakosoaji, asema Ruto
RAIS William Ruto ameungama kuwa hali nchini ni mbaya huku raia wakipitia hali ngumu kiuchumi lakini akaelezea imani kuwa serikali ya Kenya Kwanza itafaulu kukabiliana na changamoto hizo.
Alitaja mabadiliko katika bima ya afya ambapo Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF) imechukua nafasi ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) iliyovunjwa akisema itatoa huduma za afya kwa wananchi kwa gharama nafuu.
“Tulikuwa na bima ya NHIF ambayo ilishindwa kuwawezesha raia kupata huduma za afya kwa urahisi ndipo tukaiondoa na kuanzisha bima ambayo itawezesha hata watu masikini kupata huduma bora za afya. Tutawashangaza wakosoaji wetu, tutafaulu. Taifa hili halitafeli,” Dkt Ruto akasema Jumanne, Novemba 19, 2024 katika Ikulu ya Nairobi.
Kiongozi wa kitaifa pia alisisitiza kuhusu haja ya wafanyakazi wa serikali kufanya kazi kwa bidi ili waweze kufaulu akisema nguzo zote za serikali zikifaulu Kenya itakuwa imefaulu.
Rais Ruto alisema hayo baada ya kushuhudia mawaziri, makatibu wa wizara wakitia saini kandarasi ya utendakazi.
Serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikikosolewa na upinzani, mashirika ya kijamii na viongozi wa makanisa kwa kufeli kutimiza ahadi ya kuboresha uchumi wa nchi.
Wiki jana, maaskofu wa Kanisa Katoliki waliisuta serikali kwa “kuendeleaza mienendo ya kutoa kauli za uwongo” huku ikutumia vyombo vya dola kuwaandama wakosoaji wake.
Jumatatu wiki hii, Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) liliunga mkono kauli ya maaskofu hao likisema linawakilisha mawazo na maoni ya Wakenya wote milioni 50.
Akionekana kuwajibu wakosoaji wa utawala wake, Rais Ruto Jumanne alielezea kujitolea kwa utawala wake kutimiza nguzo zake nne za maendeleo.
Hizo ni ustawishaji wa sekta ya kilimo, sekta ya biashara ndogo na za kadri (MSMEs), ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, mpango wa afya kwa wote (UHC) na uchumi wa kidijitali.
“Nina uhakika kwamba tutafikia malengo hayo ya maendeleo na wanaodai kuwa tumefeli watanyamaza,” Dkt Ruto akaeleza.
Aliwaamuru mawaziri, makatibu wa wizara na maafisa wakuu wa serikali watekeleze majukumu yao bila visingizio vyovyote, akiahidi kuwa serikali itahakikisha wanapata rasilimali ili waweze kufaulu.
Kwa upande wake Naibu Rais Kithure Kindiki alisema baada ya kuchagua serikali ya Kenya Kwanza wananchi wanatarajiwa kwamba itimize hadi zake zote.
“Kwa hivyo, sote hatuna budi kushirikiana ili kufikia lengo hili,” akasema.
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alitia saini kandarasi ya utendakazi wa wizara tatu; Wizara ya Masuala ya Kigeni, Wizara ya Usalama wa Ndani na Wizara ya Jinsia, Utamaduni na Turathi.