KINAYA: Nani huyu anayemchora Zakayo akiwa mweusi kama makaa?
WAKENYA wana mchezo sana. Au pengine hawajali maisha yao. Ama hawaogopi yeyote wala chochote, au wamechoshwa na maisha, wanatafuta njia ya kuondoka Kenya na duniani haraka.
Katika nchi ambapo watu wanatekwa nyara na kutoweshwa kwa njia zisizoeleweka, wewe na akili zako timamu unaweza kuchora kibonzo cha kiongozi wako kisichompendeza?
Acha uongo wewe! Usiniambie eti hujaviona vibonzo vyeusi vinavyoenea mtandaoni vikimsawiri Zakayo kwa jinsi isiyopendeza.
Bado sijamjua mchoraji wa vizonzo hivyo vya kuchekesha na kuchukiza kwa wakati mmoja, lakini ninachojua ni kwamba yeye ni jasiri na ana bidii ya mchwa. Anafanya mambo yake kila siku.
Imekuwa desturi kwa baadhi yetu kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii mara tu baada ya kuamka, hata kabla ya kuoga wala kula staftahi, ili kuona ni mwanablogi yupi jarisi kiasi cha kuchapisha vibonzo hivyo.
Nakuhakikishia hupiti machapisho kumi yaliyopakiwa mtandaoni kila siku bila kukutana na vibonzo hivyo vyeusi, wakati mwingine vikimwonyesha Zakayo akipiga mtu teke au ngumi, au pia wakati mwingine akiwa panzi anayekula mimea!
Ninapokutana na vibonzo hivyo asubuhi nafurahia kuwa Mkenya na kujiambia kuwa bado nchi yetu haijatumbukia kwenye lindi la maangamizi kama majirani zetu Watanzania, ambao hawawezi kumdhihaki Mama Suluhu.
La ziada ni kwamba nikivipata vibonzo hivyo asubuhi humtilia dua mchoraji huyo nisiyemjua ili naye asifikiwe na kufinywa pabaya au kutoweshwa kama waandamanaji wa Gen-Z.
Wakenya tunapaswa kumshukuru Mungu sana kwa kuwa nchi yetu imekuwa na uhuru wa kuwapiga chuku viongozi wetu kwa muda mrefu.
Wakati wa utawala wa marehemu Mzee Kirungu, yule mzaliwa wa kijijini Sacho aliyetukalia mguu wa kausha kwa miaka 24, lilitokea kundi la wachekeshaji la Redykyulass lililomuiga na kumuigiza, tukaogopa sana.
Wakati huo haikuaminika kwamba yeyote nchini angemtania msema peke huyo na aendelee kupumua kwa saa zaidi ya 24.
Kumbe hatukumjua kiongozi wetu huyo! Inasemekana mwenyewe alipowaona vijana hao wakichekesha watu kwa kumuigiza alipendezwa sana, akawa shabiki wao mkuu.
Kisha? Siku moja akawaalika kula staftahi naye Ikulu ya Nairobi. Vijana hao, mmoja wao sasa ni mbunge, waliingia baridi sana walipopata mwaliko huo. Hawakujua mngetokea nini Ikulu wakifika humo.
Naambiwa Mzee Kirungu aliwapokea vyema sana, akawaandalia kahawa yeye mwenyewe kwa mikono yake, akawahimiza waendelee kuwaburudisha Wakenya kwa kumuigiza, sikwambii aliwapa na mihela kabla ya kuwasindikiza hadi mlangoni.
Ni kutokana na vichekesho vya kundi hilo ambapo tulianza kumuona Mzee Kirungu kama binadamu mwenzetu, tukaacha kumwogopa, tukasahau propaganda zilizomsawiri kama jini-mtu!
Ningekuwa Zakayo, ningewatuma wasaidizi wangu wamtafute mchoraji vibonzo hivyo vyeusi kama kaniki, nimfanye rafiki yangu, aache kunichora nikifanya ya hovyo.