Jinsi ukuruba wa Ruto na kanisa unavyoyeyuka upesi; je, atanusuru ‘baraka’?
RAIS William Ruto anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa kidini hivi kwamba sadaka yake inakataliwa huku akikosolewa vikali na waliomuunga mkono wakati wa kampeni za 2022.
Kiongozi wa nchi sasa amekosa faraja kwa kanisa ambalo lilikuwa msingi wa kampeni zake mnamo 2022. Alipotua mamlakani, baadhi ya viongozi wa makanisa ambao walikuwa mrengo wa Ruto walitaja utawala wake kama wa Mungu.
Tukio la Jumatatu usiku ambapo Askofu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Nairobi Philip Anyolo aliamrisha karibu Sh6 milioni ambazo Rais alitoa Jumapili arejeshewe, linaonyesha jinsi kanisa linavyoendelea kuondoa ‘baraka’ na ‘upako’ kwa Rais.
Askofu Anyolo kwenye barua, aliagiza Rais arejeshewe pesa hizo alizotoa na nyingine alizoahidi alipohudhuria ibada kwenye Kanisa Katoliki la Soweto eneobunge la Embakasi Mashariki.
Aidha, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja pia hakusazwa kwa kuwa Sh200,000 alizotunuku kwaya ya kanisa hilo pia atarejeshewa, tukio ambalo linaendelea kushabikiwa na umma, hasa vijana.
Pesa zitarejeshwa
“Pesa hizi zitarejeshwa kwa waliozitoa. Wanasiasa wanakaribishwa kanisani ili kulishwa chakula cha kiroho lakini wanashauriwa wafanye hivyo kama waumini wengine,” ikasema sehemu ya taarifa ya Askofu Anyolo.
“Hii itahakikisha kuwa hawatumii nyadhifa zao kwa manufaa ya kisiasa,” ikaongeza taarifa hiyo.
Japo kuna marufuku ya michango ya harambee ambayo ilitolewa Julai 5, wikendi Rais na Naibu wake Profesa Kithure Kindiki walionekana kurejelea matoleo makubwa kanisani.
Profesa Kindiki alitoa jumla ya Sh7 milioni ambazo Sh5 milioni zilikuwa kutoka kwa Rais Ruto na zake Sh2 milioni, pesa ambazo alizirejelea kama sadaka na si mchango wa harambee ambayo ni marufuku.
Kabla ya tukio la sadaka ya Rais kukataliwa, Baraza la Maaskofu wa Katoliki Nchini (KCCB) wiki jana lilitoa taarifa ambayo iliacha idara mbalimbali za serikali zikiharakisha kutuma taarifa za kujitetea.
Baraza hilo lenye maaskofu 26 lilitumia maneno makali kumshambulia Rais na utawala wake, likimrejelea kama kiongozi ambaye ana mazoea ya kudanganya wakati Wakenya nao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Wakenya wanastahili kujifunza kutoshangilia uongo ambao wanasiasa wanawaambia na waamue kusaka na kuongozwa kupitia ukweli,” akasema Askofu wa Dayosisi ya Eldoret Domnic Kimengich.
Kupora pesa
“Ufisadi si lazima uwe kupora pesa ila kutumia afisi yako vibaya. Unafiki ambao tunauona ndani ya serikali unasikitisha sana,” akasema Mwenyekiti wa KCCB Maurice Muhatia.
Maaskofu hao walidai kuwa, serikali inahusika na utekaji nyara ambao umezidi na pia kuwahangaisha Wakenya kupitia Bima ya Afya ya Jamii na mfumo wa kibaguzi wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Kando na matoleo yake kukataliwa na kanisa Katoliki, viongozi wengine wa kidini waliokuwa wandani wa Rais 2022 wamemruka wakimlaumu kwa uongozi mbaya.
Mwiinjilisti Teresiah Wairimu ambaye alikuwa na ukuruba na familia ya Rais na aliongoza ibada kwenye makazi yake akiwa naibu rais, mnamo Oktoba 27 alimgeuka.
“Nilifikiria kuwa hii ni serikali ya Mungu kwa sababu ndiyo tuliichagua lakini imetuabisha na ni serikali ya vita.
Katika uchaguzi mkuu unaokuja lazima mtu aende nyumbani na watu lazima waanze kuenda nyumbani,” akasema Bi Wairimu.
Askofu wa Kianglikana, Jackson Ole Sapit ambaye alitakasa ‘ushindi’ wa Rais Ruto ukumbi wa Bomas pia amemgeuka akisema hakuna vitisho vitakavyowazuia kuanika maovu ya Rais Ruto na utawala wake.
Kuwaambia ukweli
“Tutazidi kuwaambia walio mamlakani ukweli,” akasema Askofu Sapit akiwaunga wenzake wa KCCB.
Hata katika ngome ya Kinara wa Upinzani Raila Odinga ambako Rais Ruto anategemea kupata uungwaji mkono, viongozi wa kidini Jumapili walimwaambia utawala wake umeoza na wakatishia kuongoza raia kususia kulipa ushuru.
“Hata viongozi wa hapa wakinyamaza kwa sababu Raila anashirikiana na Rais, sisi tutazungumzia maovu ya utawala huu ambao unawanyanyasa Wakenya na kufanya maisha yawe magumu,” akasema Askofu wa ACK Bondo David Kodia.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo amesema Rais hana lake iwapo ataendelea kukosolewa na makanisa.
“Makanisa yanamsukuma ahakikishe kuwa sera zake dhalimu zinabadilishwa hasa zile zinazogusia sekta ya afya ambapo makanisa yana hospitali kadhaa. Makanisa pia yana haki ya kukosoa serikali lakini sasa mahali inapoelekea, yamechukua jukumu la upinzani ambao sasa haupo,” akasema Bw Bigambo.
“Kanisa lina ushawishi mkubwa hasa mashinani na busara anayohitaji Ruto ni kutekeleza sera zake kwa njia ambayo inaboresha maisha ya Wakenya. Iwapo atakiuka hili, hao maaskofu huenda wakashawishi raia wasimpigie kura 2027,” akaongeza.