Hakuna Ndege michezoni:Wetang’ula asema wabunge watatumia SGR kwenda Mombasa
WABUNGE watakaoshiriki katika michezo baina ya wabunge wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), watasafiri Mombasa kwa gari moshi sio kwa ndege kama ilivyo kawaida yao,ametangaza
Kwenye taarifa bungeni Jumanne alasiri, Bw Wetang’ula alisema hata yeye atasafiri kwa SGR.
Kulingana na Spika huyo, hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya nguzo hiyo ya serikali kupunguza gharama ili kuelekeza pesa kwa mipango inayofaidi raia moja kwa moja.
“Nawaalika Mombasa kwa michezo baina ya mabunge ya EALA ambapo wabunge kutoka mataifa manane wanachama watashiriki. Nyie, pamoja na Spika, mtasafiri kwa SGR. Kwa wale ambao mtasafiri, mpange na afisi ya karani wa bunge kuhusu siku ambayo mtaondoka Nairobi kuelekea Mombasa,” Bw Wetang’ula akaeleza.
Michezo hiyo, inayoshirikisha fani mbalimbali, imeratibiwa kuanza Desemba 6, 2024 hadi Desemba 18, 2024.
Bw Wetang’ula aliongeza kuwa uamuzi wa kutumia SGR utaisaidia bunge kulipia gharama za wabunge wengi watakaoshiriki katika michezo hiyo ya EALA.
Kiongozi wa wengi, Bw Kimani Ichung’wah alisema anaunga mkono uamuzi kwamba wabunge wasafiri Mombasa kwa gari moshi.
“Tutaungana na Spika ambaye ataabiri SGR kuelekea Mombasa mnamo Desemba 6 saa kumi na mbili alfajiri. Kwa sababu sisi ndio wenyeji, wabunge wote 349 wanatarajiwa kuwa Mombasa,” akaeleza Mbunge huyo wa Kikuyu.
Hata hivyo, wabunge wengine walisikika wakinung’unika ishara ya kutofurahishwa na pendekezo hilo la Spika Wetang’ula.
Mnamo Julai mwaka huu serikali ililazimika kupunguza mgao wa bajeti kwa matawi yote matatu ya serikali baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 uliotarajiwa kuiwezesha serikali kukusanya Sh346 bilioni zaidi.