Lugha, Fasihi na Elimu

Miswada inayokusudiwa kutumiwa kushirikisha umma katika maamuzi ya kisheria itafsiriwe kwa Kiswahili

Na IRIBE MWANGI November 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAMATI inayohusika na masuala ya fedha bungeni “inapokea maoni kutoka kwa wananchi” kuhusu Mswada unaokusudia kufanya marekebisho katika sheria inayohusu ushuru.

Jijini Mombasa, mzee mmoja alizungumza na kujibu maswali niliyoyauliza kuhusu kamati iyo hiyo mnamo tarehe 6 mwezi wa sita mapema mwaka huu. Alisema kwamba ilikuwa vigumu kuchangia kikamilifu Mswada ulioandikwa kwa Kiingereza ambacho hakukielewa vizuri. Alitamani lau mswada huo ungeandikwa kwa Kiswahili! Naomba niyarudie niliyoyasema kwa kamati hiyo japo kwa marekebisho kiasi.

Ukusanyaji huu wa maoni unafanyika ili kutimiza matakwa ya Katiba. Swali langu ni, je, hawa wananchi wanahusishwa kihalisia au kinadharia tu? Nafikiri mzee huyo alinipa jibu la swali hilo. Mbali na “wataalamu” na mashirika je, umma umeshirikishwa kama inavyowaziwa na Katiba? Nashangaa kama Bunge limetia jitihada yoyote katika kumhusisha “mwendesha bodaboda, mama mboga na Wanjiku” kwa kumfanya aelewe yaliyomo katika Mswada huo unaohusu ushuru.

Kwa hakika, Mswada huu hauwezi kueleweka kwa urahisi hata kwa watu waliosoma hadi chuo kikuu kama hawakuzingatia masomo ya fedha. Kama ilivyo miswada yote, umetumia lugha ya “kuwafungia nje” wengi. Ni udanganyifu kusema kwamba unawahusisha watu katika mjadala utumiapo lugha wasiyoielewa kama alivyoashiria mzee huyo.

Maoni yangu ni kwamba kama kuna nia ya kuhusisha umma katika maamuzi haya yanayohusu ushuru, basi sera na miswada sharti itafsiriwe kwa lugha na kwa namna itakayoeleweka na wengi.  Kama lugha asilia hazitatumika, hakuna sababu yoyote ya kukosa kutafsiri miswada yote inayojadiliwa kwa Kiswahili – lugha ya taifa na rasmi. Bunge kazi kwenu!