Yafichuliwa kwa miezi tisa tu, Wakenya walituma Sh7 trilioni kwa simu
KIASI cha pesa zilizotumwa na Wakenya kupitia simu za mkononi kiliongezeka kwa asilimia 13.2 katika miezi tisa iliyomalizika Septemba 2024 ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka jana, hali iliyochochewa na kubadilishwa kwa sera ya kutuma pesa ya kampuni ya Airtel mwezi Februari.
Takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha kuwa Wakenya walituma Sh6.5 trilioni kupitia majukwaa ya pesa za kielektroniki katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu, ikilinganishwa na Sh5.8 trilioni mwaka jana.
Ongezeko hilo, ni tofauti na kushuka kwa asilimia 2.7 katika kipindi cha miezi tisa kilichomalizika Septemba mwaka jana, na lilijiri wakati Airtel Kenya ilipofuta kanuni iliyowalazimu wateja wanaotumia huduma ya Airtel Money kutoa pesa ndani ya wiki moja baada ya kupokelewa.
Kampuni hiyo ya simu ya pili kwa ukubwa nchini Kenya ilifanya mabadiliko hayo ndoa Februari mwaka huu, hivyo kuruhusu wateja wa Airtel Money kupokea pesa moja kwa moja kwenye pochi zao za kielektroniki kutoka mtandao wowote.
Mwaka huu, wateja walituma na kupokea kiwango cha juu zaidi cha pesa mnamo Februari cha Sh790.8 bilioni, huku cha chini kikikiwa Septemba, Sh 670.52 bilioni.
M-Pesa ndio jukwaa kuu la kutuma pesa kwa njia ya simu nchini, ikiwa na asilimia 93.4 kufikia Juni 2024, ikifuatiwa na Airtel Money kwa asilimia 6.6.
Matumizi ya pesa kwa simu ya mkononi yamedumisha umaarufu wake nchini Kenya kwa miaka mingi, yakichochewa na kuongezeka na huduma bora za mtandao na mawasiliano ya simu na vile vile urahisi wa watumiaji kutuma na kupokea pesa.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA