Adani, ambaye Serikali ya Kenya inataka asimamie JKIA, ashtakiwa kwa ufisadi Amerika
BILIONEA Gautam Adani, mwenyekiti wa kampuni kubwa ya Adani Group kutoka India ambayo serikali ya Kenya imepatia kandarasi za mabilioni ya pesa na mmoja wa watu tajiri zaidi duniani, amefunguliwa mashtaka ya ufisadi jijini New York, Amerika.
Adani anadaiwa kuhusika katika hongo ya mabilioni ya dola na udanganyifu, waendesha mashtaka wa Amerika walisema Jumatano.
Walisema Adani na washtakiwa wengine saba, ikiwa ni pamoja na mpwa wake Sagar Adani, walikubali kulipa hongo ya takriban dola 265 milioni (Sh35 bilioni) kwa maafisa wa serikali ya India ili kupata kandarasi za zaidi ya dola 2 bilioni kuhusiana na kandarasi ya kuendeleza mradi mkubwa zaidi wa umeme wa jua nchini India.
Hakuna aliye kizuizini
Waendesha mashtaka pia walisema Adani na afisa mkuu wa kampuni tanzu ya Adani Green Energy, Mkurugenzi Mtendaji wa zamani Vneet Jaain, walikusanya zaidi ya dola 3 bilioni za kuficha ufisadi wao kutoka kwa wakopeshaji na wawekezaji.
Kulingana na shtaka, baadhi ya watu waliokula njama walimtaja Gautam Adani faraghani kwa majina ya “Numero uno” na “mtu mkubwa,” huku Sagar Adani akidaiwa kutumia simu yake ya rununu kufuatilia hongo hiyo.
Kampuni hiyo na ubalozi wa India huko Washington haukujibu mara moja maombi ya kutoa maoni kwa Reuters na mawakili wa washtakiwa hawakuweza kufahamika mara moja.
Gautam Adani, Sagar Adani na Jaain walishtakiwa kwa ulaghai, njama ya ulaghai, na njama ya ulaghai wa kielektroniki.
Washtakiwa wengine watano walishtakiwa kwa kula njama ya kukiuka Sheria ya Ufisadi, sheria ya Amerika dhidi ya rushwa, na wanne walishtakiwa kwa kula njama kuzuia haki.
Hakuna hata mmoja wa washtakiwa aliye kizuizini, msemaji wa Mwanasheria wa Amerika Breon Peace huko Brooklyn alisema. Gautam Adani anaaminika kuwa yuko India.
Wengine ambao walishtakiwa kwa jinai Jumatano ni pamoja na Ranjit Gupta na Rupesh Agarwal, Mkurugenzi Mtendaji wa zamani na afisa mkuu wa zamani wa mikakati na biashara wa Azure Power Global, ambayo mamlaka ilisema ilikubali kulipa baadhi ya hongo.
Kushtakiwa kwake kunajiri siku chache baada ya serikali ya Kenya kutetea kandarasi ambazo imetoa kwa kampuni hiyo.
Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga na mawaziri Davis Chirchir na John Mbadi wametetea mikataba ya Kenya na kampuni hiyo licha ya kupingwa kortini.
Bw Chirchir aliambia wabunge kwamba Adani, ambayo imewasilisha zabuni ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kima cha Sh230 bilioni, na hivi majuzi ilitia saini mkataba mwingine wa kawi wa Sh96 bilioni wa miaka 30 na Kenya, haijapigwa marufuku katika nchi yoyote ile na inalipa ushuru kikamilifu.
Waziri aliambia Bunge kwamba kulingana na uchunguzi uliofanywa na serikali ya Kenya, Adani haijajihusisha na vitendo vyovyote vya ufisadi na haijafilisika.
“Adani haijajihusisha na ufisadi hadi sasa, haijafilisika na inazingatia ulipaji wa kodi kote, haijakosea katika uwajibikaji wake kwa jamii na ajira na wakurugenzi wake hawajapatikana na hatia kwa kosa lolote linalohusiana na maadili ya kitaaluma katika kipindi cha miaka mitano kabla ya kuwasilisha pendekezo lao,” Bw Chirchir alisema mbele ya kamati ya bunge akitetea uamuzi wa Kenya wa kutia mkataba wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na kampuni hiyo.