Michezo

Nyota wanne warejea kikosini kupiga jeki Manchester City

Na MASHIRIKA November 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MABINGWA watetezi Manchester City wanatarajiwa kukaribisha nyota wanne kwa mechi kali ya Ligi Kuu dhidi ya Tottenham Hotspur ugani Etihad hapo kesho.

Mshambulizi Jack Grealish alikuwa katika orodha ya wachezaji waliowapa City wasiwasi, alionekana akifanya mazoezi Jumatano.
Grealish hajachezea City tangu atumiwe kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Wolves hapo Oktoba 20.

Licha ya kulazimika kukosa michuano dhidi ya Sparta Prague (Oktoba 23), Southampton (Oktoba 26), Tottenham (Oktoba 30), Bournemouth (Novemba 2), Sporting (Novemba 5) na Brighton (Novemba 9) kwa sababu ya jeraha, Grealish alijumuishwa katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Uingereza cha kocha Lee Carsley kilichoshiriki mechi za Ligi ya Mataifa ya Ulaya dhidi ya Ugiriki na Ireland.

Hata hivyo, Grealish alikuwa katika orodha ya wachezaji tisa waliojiondoa katika kikosi cha Carsley kabla ya mechi hizo, hatua hiyo ikimpa muda wa kupona kabisa kabla ya ratiba ngumu ya klabu.
Anatarajiwa kurejea uwanjani kwa mashindano baada ya kuchapisha picha kwenye Instagram akifanya mazoezi na wachezaji wenza wa City.

Picha hiyo iliandamana na ujumbe wa kutia moyo.
“Hatimaye nimeungana tena na kikosi,” akasema Grealish, 29, anayeaminika kumezewa mate na Spurs.
Grealish atatumai kusaidia City kuanza kushinda tena baada ya vichapo dhidi ya Spurs 2-1 (Kombe la Carabao), Bournemouth 2-1 na Brighton (ligini) na Sporting 4-1 (Klabu Bingwa Ulaya).

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola akitoa usia kwa Bernardo Silva na Ilkay Gundogan katika mechi ya awali. Picha|Reuters

Mbali na Grealish, mabeki John Stones na Manuel Akanji, na kiungo Kevin De Bruyne walifanya mazoezi Jumatano, na kumpa kocha Pep Guardiola motisha kubwa.

Stones amekosa mechi tatu akiwa na jeraha la wayo, naye De Bruyne alishiriki michuano miwili iliyopita kutoka kwenye benchi kabla ya majukumu ya timu ya taifa baada ya kuwa mkekani na jeraha la msuli.

Akanji hakushiriki mechi za timu yake ya taifa ya Uswisi baada ya kutumiwa kama mchezaji wa akiba dhidi ya Brighton.
City wataingia katika mchuano huo wao wa 12 wakishiriki nafasi ya pili kwa alama 23, tano nyuma ya viongozi Liverpool, nao Tottenham wanapatikana nambari 10 kwa alama 16.

Aidha, Tottenham wamekata rufaa dhidi ya marufuku ya mechi saba aliyopokezwa kiungo Rodrigo Bentancur. Nyota huyo aliadhibiwa na Shirikisho la Soka nchini Uingereza (FA) mnamo Jumatatu kwa matamshi yake dhidi ya mchezaji mwenzake Son Heung-min raia wa Korea Kusini.

Akizungumza kwenye runinga ya Uruguayan TV, Bentancur alitoa maneno yasiyo adilifu kuhusu Wakorea baada ya kuulizwa swali kuhusu Son yaliyoenea kwenye mitandao ya kijamii kabla ya msimu huu kuanza.