Habari za Kitaifa

Ruto ahimiza ‘Boy Child’ akuzwe vyema kuepuka visa vya ukatili dhidi ya wanawake

Na BENSON MATHEKA November 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amewataka wazazi kote nchini kujitahidi zaidi kuwalea vyema watoto wavulana ili kusaidia kukabiliana na visa vya mauaji ya wanawake nchini.

Akizungumza bungeni wakati wa hotuba ya kila mwaka, Ruto alikariri umuhimu wa kuwafunza wavulana maadili mema kuanzia wakiwa wadogo ili kuwaepusha kukua na kuwa wahusika wa unyanyasaji wa kijinsia.

“Ni wakati wa kila mmoja wetu, kutekeleza jukumu letu katika kuwalea wavulana kuwa wanaume waadilifu ambao hawatahitaji kuthibitisha uanaume wao kwa gharama ya wanawake,” Ruto alisema.

Rais alisisitiza usawa kati ya jinsia hizo mbili akisema wanawake sio raia duni.

Ili kupata suluhu la kudumu kwa uovu huo, Ruto alisema kuwa amehusisha viongozi wanawake katika mijadala na akampa Naibu Rais Kithure Kindiki jukumu la kuongoza mashauriano hayo.

“Nimefanya majadiliano na viongozi wengine serikalini na nimempa Naibu Rais jukumu la kuwezesha majadiliano ya ushirikiano, mapana na ya sekta mbalimbali na kupendekeza hatua madhubuti ndani ya miezi sita,” alisema.

Hotuba yake ilijiri siku moja tu baada ya kutoa matamshi sawa na hayo alipokutana na viongozi wanawake kujadili visa vilivyokithiri vya mauaji ya wanawake ambavyo vimekuwa vikisumbua taifa.

Katika hotuba yake Jumatano, Ruto alisisitiza kuwa serikali inaunga mkono wanawake kikamilifu na atahakikisha wote waliohusika na mauaji hayo wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Nirudie tena kwamba serikali, katika ajenda yake ya wanawake, imejitolea kwa uwazi kukomesha aina zote za ukatili. Kama viongozi, tumeungana katika azma ya kuhakikisha kuwa haki inafanyika haraka na kwa ufanisi,” aliongeza.

Ili kuendeleza ajenda hii, Ruto alitangaza kuwa Sh100 milioni zimetengwa kwa kampeni ya kila mwaka ya siku16 dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Kampeni ya mwaka huu iliyopewa jina la Nyumba Salama, Nafasi Salama itaanza Jumatatu, Novemba 25, na itaendelea kwa siku 16.

“Ninaomba kila Mkenya ajiunge katika harakati hizi za kupaza sauti, kuelimisha, na kusimama kidete kupinga visa vya mauaji ya wanawake. Jamii zetu zinahitaji elimu kuhusu dalili na visababishi vya unyanyasaji na rasilimali zinazopatikana kwa waathiriwa,” Rais Ruto alisema, akiwaalika Wakenya kushiriki katika kampeni hiyo.