Watu watano wafariki kwenye ajali Kirinyaga, mmoja ajeruhiwa
WATU watano Ijumaa walifariki huku mmoja akipata majeraha mabaya katika ajali iliyotokea kwenye barabara ya Sagana – Karatina, Kaunti ya Kirinyaga.
Ajali hiyo ilitokea baada ya trela iliyokuwa imebeba mahindi kugonga magari mawili ya kibinafsi katika soko la Kibirigwi, eneobunge la Ndia.
Kulingana na walioshuhudia, trela ilipoteza mwelekeo baada ya breki kufeli. Trela hiyo iliyumbayumba barabarani na kugonga gari dogo aina ya Mazda Supremacy kutoka nyuma upande wa kulia na kuua watu wanne waliokuwa ndani.
Huku trela hiyo ikiteremka barabarani, iligongana ana kwa ana na gari jingine aina ya Toyota Corolla na kuiburura kwa mita chache kabla ya kuligongesha mtaroni.
Kwa masikitiko makubwa dereva wa gari hilo alifariki papo hapo akishikilia usukani.
Dereva wa wa trela aliyetambuliwa kwa jina Daniel Muriungi aliponea kifo na akapelekwa katika zahanati ya Kibirigwi kwa matibabu. Baadaye alisafirishwa hadi hospitali ya Karatina kwa matibabu maalum hali yake ilipodorora.
Miongoni mwa waliofariki ni mwanamke aliyesafiri kwa gari aina ya Mazda Supremacy. Mkuu wa Polisi wa Kirinyaga Magharibi Moses Koskei amesema uchunguzi wa ajali hiyo umeanza.
Miili ya walioaga dunia ilipelekwa katika makafani ya hospitali ya rufaa ya Kerugoya ikisubiri kufanyiwa uchunguzi wa postmortem huku magari yaliyoharibika yakivutwa hadi katika kituo cha polisi cha Sagana kwa ukaguzi.
“Ilikuwa ajali mbaya sana kwa sababu watu watano wamefariki papo hapo na hata hakukutokea nafasi zozote ambayo ingechangia kuokolewa kwao,” akasema Bw Githiru Wanjohi, mkazi wa eneo.
Bw Munene Kariuki aliyefika katika eneo la ajali baada ya kusikia sauti ya kitu kilichoanguka alisikitikia mauti hayo na jinsi tukio lenyewe lilivyofanyika.
“Nilipofika katika eneo la ajali ambapo miili mitano ilikuwa imekwama, nilihuzunika sana.” akasema.
Polisi wakisaidiana na wakazi walikata vyuma vya magari ili kuopoa miili iliyokwama ndani ya magari yaliyobondeka. Katika eneo la ajali, magunia ya mahindi yalitapakaa kila mahali huku polisi wakiyalinda yasiibwe
Bw Koskei alishauri madereva wawe waangalifu wanaposafiri katika barababara hiyo waepuke ajali mbaya kama hii hasa msimu huu ambapo watu watakuwa wakianza kuingia mwezi wa sherehe.
“Dereva wa trela alipiga honi mfululizo alipogundua amepoteza usukani wa gari lake lakini madereva hawakumchukulia kwa uzito,” alisema Bw Koskei.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan