Sheria: Utanyimwa haki ya kulea mtoto wako ukitekwa na dawa za kulevya
UTANYIMWA haki ya kulea mtoto wako iwapo wewe ni mraibu wa dawa za kulevya na ikithibitisha una mazoea ya kuwanyanyasa, sheria ya watoto inasema.
Kulingana na sheria hiyo,watoto walio na umri wa chini ya miaka 10, ni mama zao wanaopatiwa haki ya malezi isipokuwa kama imethibitishwa kuwa hawezi kuwalea kutokana na masuala kama vile unyanyasaji, kuwatelekeza, wana ugonjwa wa akili usiotibika, au ni waraibu wa dawa za kulevya.
Nchini Kenya, sheria kuhusu malezi ya mtoto zinapatikana katika Sheria ya Watoto ya 2022, ambayo inabainisha haki na wajibu wa wazazi, walezi, na serikali kuhusiana na watoto.
Masuala ya malezi ya mtoto mara nyingi hutokea wazazi wanapotengana au kuachana. Sheria nchini Kenya inatambua kwamba maslahi ya mtoto ni muhimu katika uamuzi wowote ambao anahusika.
Wakati wa kufanya uamuzi kuhusu ni nani anapaswa kuishi na kumlea mtoto, mahakama huzingatia mambo mbalimbali hasa umri wa mtoto, afya yake na na uwezo wa mzazi wa kukidhi mahitaji ya mtoto. Katika baadhi ya matukio, mtoto anaweza kuruhusiwa kuamua anayetaka kuishi naye kati ya baba na mamake iwapo ana umri wa kutosha.
Katika sheria, malezi ya mtoto ni uhusiano kati ya mzazi au mlezi na mtoto. Sheria inafafanua haki na wajibu wa mzazi kufanya maamuzi kuhusu malezi ya mtoto. Inajikita kuhakikisha anaishi mahali pazuri, salama na anaweza kupata elimu
Mahakama inaweza kugawanywa malezi ya mtoto kwa baba na mama wakitengana: Malezi ya pamoja yanamaanisha kwamba wazazi wote wawili wana haki ya kufanya maamuzi kuhusu maisha ya mtoto wao, malezi ya pekee yanamaanisha kwamba ni mzazi mmoja tu ndiye ana haki ya kufanya maamuzi kuhusu maisha ya mtoto wake.
Kutwikwa jukumu la malezi ya mzazi mmoja, ina maana kwamba mzazi mmoja ataishi na mtoto na kuwa mlezi mkuu na mtoa maamuzi. Hata hivyo, asiyetwikwa jukumu hili, awe baba au mama, anaweza kupatiwa haki ya kumuona na kumtembelea mtoto mara kwa mara.
Mahakama inaweza pia kuweka au kuidhinisha mpangilio maalum wa malezi ambapo wahusika, kupitia mpatanishi au wakili, wanakubaliana jinsi wanavyotaka kushiriki malezi.
Ni muhimu kutambua kwamba maamuzi ya malezi yanaweza kurekebishwa ikiwa kuna mabadiliko makubwa katika hali zinazoathiri ustawi wa mtoto.
Ni muhimu kusisitiza kuwa katika kuamua kuhusu malezi, mahakama huzingatia maslahi bora ya mtoto.
Sheria ya Watoto, 2022 inatwika mahakama mamlaka ya kutoa haki ya kutunza watoto kulingana na ukweli na ushahidi uliopo ili kuhakikisha suluhu bora zaidi kwa maisha na usalama wa mtoto.
Sababu nyingine ambayo inazingatiwa ni hali ya maisha ya kila mzazi na uwezo wao wa kuandaa mazingira ya nyumbani yenye utulivu kwa mtoto. Hii ni pamoja na mambo kama vile tabia ya mzazi na hali ya makazi ili kuepuka kumweka mtoto katika mazingira yanayoweza kumdhuru.
Mahakama inaweza pia kuzingatia historia yoyote ya unyanyasaji au kutelekezwa na mzazi yeyote, pamoja na historia yoyote ya uhalifu.
Sheria inayosimamia malezi ya mtoto nchini Kenya inatambua kwamba wazazi wote wawili wana haki sawa za malezi, lakini mahakama inaweza kutoa haki kwa mzazi mmoja iwapo mzazi mwingine atapatikana kuwa hafai au hawezi kuweka mazingira salama na thabiti kwa mtoto.