Mbinu hizi zitakusaidia kuboresha burundani chumbani
USIJIRUSHE tu kitandani na usubiri mchumba wako ukitarajia burundani ya kukata na shoka. Shughuli za chumbani zinahitaji maandalizi ya kishua. Sio kuparamiana.
Unapoenda kulala hakikisha uko msafi na sio kuwa na uvundo wa jasho na mdomo. Kwa kudumisha usafi unamsisimua mwenzi wako kufanya mapenzi na wewe.
Kabla ya kuingia kitandani, elewa hali ya mwenzako kihisia na ikiwezekana, usiache mtu wako akiendelea na shughuli za nyumbani ukamsubiri aje kukuandalia burundani akiwa mchovu.
Msaidie kwa hizo shughuli mkipiga gumzo kuhusu mapenzi. Utakuwa ukimuandaa kisaikolojia kwa burundani unayotarajia. Hakikisha mtu wako hakushuku kwa kuchepuka.
Njia ya haraka ya kuharibu raha ya chumba cha ndoa ni mwenzi wako kushuku kuwa una mipango ya kando.
“Haitoshi kuwa mwaminifu, mwenzi wako lazima pia atambue kwa uhakika kuwa wewe ni mwaminifu,” asema Daisy Kalunde, mshauri wa masuala ya mapenzi.
Anasema kwamba watu wanavuruga raha ya chumbani kwa kurudi nyumbani kuchelewa . Hulka hii, aeleza, inapunguza uaminifu.
“ Mazoea ya kuchelewa kufika nyumbani bila sababu maalumu hasa kwa wanawake na kulala nje kwa wanaume ni sumu kali ya kuua ndoa,” asema.
Usianze kung’orota bila kujua iwapo mwenzi wako anakuhitaji. Zoea kumtakia usiku mwema na kumwamkua asubuhi ikiwezekana kwa busu. Maneno good night na good morning ni rahisi lakini muhimu kwa uhusiano wa mtu na mchumba wake.
Vaa kwa starehe ya chumbani. Vaa mavazi ya kumsisimua na kuleta shangwe kwa burundani. Kumbuka chumba cha kulala cha wanandoa ni cha watu wawili wanaopaswa kuchangamshana.
Ikiwa unavaa kuvutia ukiwa kazini, basi unapaswa kufanya hivyo chumbani kumpagawisha mtu wako. Jifunze kumfanyia mtu wako mambo madogo ya kumtia shime kwa shughuli chumbani; mdekeze, mbusu, mguse lakini usilazimishe burundani.
“Unapoona mwenzi wako amechoka, mruhusu apumzike na mzungumze wakati nyinyi wawili mko freshi. Onyesha kwamba unaelewa.
Epuka kuchat na watu kwenye simu usiku ukiwa na mwenzi wako, epuka TV na mitandao ya kijamii pia ukiwa chumbani,” asema Kalunde.
Usitarajie mambo kuwa sawa chumbani kati yenu ikiwa umekuwa ukimtendea mwenzi wako vibaya na kwa jeuri wakati wa mchana.
Ikitokea nyinyi wawili hamko kama mlivyozoea, usilalamike na kumshambulia mwenzi wako kwa mabadiliko hayo.
Badala yake, mvutie mwenzi wako arudi kwako hatua kwa hatua. Watu wanavutiwa na uzoefu ambao ni salama na mwepesi, sio wa kulazimishwa.