Jamvi La Siasa

Kutekwa nyara kwa Besigye: Uganda ilivyoanika uongo wa Kenya

Na  BENSON MATHEKA November 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UGANDA imeanika uongo wa Kenya kuhusiana na kutekwa nyara kwa kiongozi wa upinzani nchini humo Kizza Besigye akiwa jijini Nairobi.

Kenya ilikanusha kuhusika na kutekwa nyara kwa Besigye ikisema maafisa wake wa usalama hawakuhusika.

Hata hivyo, kulingana na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Uganda, Chris Baryomunsi, seŕikali ya Kenya ilifahamu kuhusu oparesheni hiyo.

Baryomunsi amedai kuwa operesheni kama hiyo isingeweza kutokea bila Kenya kujua, na hivyo kuzua mjadala mkali kuhusu jukumu la serikali ya Kenya  katika suala hilo lilizua lawama kimataifa.

Akizungumza na Televisheni ya NBS mnamo Ijumaa, Novemba 22, Baryomunsi alidai kuwa utekaji nyara wa Besigye kutoka Nairobi hadi Uganda unamaanisha ushirikiano katika ngazi za juu. “Unawezaje  kumkamata mtu Nairobi na kisha kumrudisha Uganda bila Kenya kujua?” alisema.

Besigye, mkosoaji mkubwa wa Rais Yoweri Museveni, alitoweka akiwa jijini Nairobi Jumamosi Novemba 16.

Siku kadhaa baadaye, aliibuka tena nchini Uganda, akikabiliwa na mashtaka ya kumiliki silaha kinyume cha sheria katika mahakama ya kijeshi.

Mkewe, Winnie Byanyima, alisema mashtaka hayo  ni ya uongo, akifafanua kuwa kwa miongo miwili Besigye hajamiliki silaha

Kutekwa kwa Besigye kumefanya Kenya  kumulikwa kimataifa kwa jinsi inavyoshughulikia raia wa  kigeni hasa viongozi wa upinzani wa nchi zingine.

Hafla ya Martha Karua

Martha Karua, ambaye aliandaa hafla ambayo Besigye aliratibiwa kuhudhuria, alishutumu serikali ya Kenya kwa kuwezesha kutekwa nyara  mwanasiasa huyo wa Uganda. “Tunashuku kwamba serikali ya Uganda ilifanya kazi kwa kusaidiwa na Kenya,” alisema

Katibu wa Masuala ya Kigeni Korir Singoei alisema serikali  ya Kenya haikuhusika na utekaji nyara wa Besigye.

“Kutokana na ripoti ninazopokea, ni kwamba Besigye alitekwa nyara kutoka jengo moja jijini Nairobi. Ukweli, hata hivyo, ni kwamba hiki si kitendo cha serikali ya Kenya. Si kitendo cha maafisa wetu wa usalama,” Singoei aliambia runinga ya Citizen Jumatano usiku.

Kulingana naye, serikali haikufahamu kuhusu ziara ya Besigye  nchini. Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Uganda alisisitiza kwamba kukamatwa kwa aina hiyo kunahusisha ushirikiano na nchi mwenyeji, na hivyo kuashiria kuhusika kwa Kenya.

Umoja wa Mataifa walaani

Umoja wa Mataifa umelaani tukio hilo, huku mkuu wa haki za binadamu Volker Turk akitaka Besigye aachiliwe na Uganda  kukomesha  kuwashtaki raia katika mahakama za kijeshi.

Amerika pia imechukua tahadhari, huku Seneta James Risch akihoji jukumu la Kenya katika suala hilo. “Tukio hili linazua maswali mazito kuhusu heshima kwa kanuni za kimataifa,” aliandika kwenye X, akihimiza uwazi kutoka kwa mataifa yote mawili.