Habari za Kaunti

Kuna mvua katika maeneo haya kwa siku tano zijazo

Na BENSON MATHEKA November 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA katika maeneo ya Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Nyanda za Juu Kusini-mashariki, eneo la Pwani,Kaskazini-Magharibi na Kaskazini- Mashariki mwa Kenya wameshauriwa kujiandaa kwa mvua katika siku kadhaa zijazo.

Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya imetangaza kuendelea kunyesha kwa mvua katika maeneo haya pamoja na Nairobi kuanzia Ijumaa, Novemba 22, hadi Jumanne, Novemba 26.

Katika ushauri wake kuhusu mvua wikendi, idara ilifichua kuwa mvua kubwa itanyesha katika baadhi ya maeneo hayo.

Kulingana na idara hiyo mvua ya wastani hadi kubwa inatarajiwa katika kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka Nithi na Nairobi.

Wakenya wanaoishi katika maeneo yaliyotajwa walishauriwa wajihadhari na uwezekano wa mafuriko huku mvua hiyo ikitarajiwa kuanza alasiri na kuendelea hadi usiku.

Kaunti za Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru na Narok pia zimeorodheshwa miongoni mwa kaunti zilizokuwa na mvua kubwa.

Kaunti zingine ni miongoni mwa maeneo ya Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Pokot Magharibi ambako mvua itanyeshak mchana.

Hata hivyo, Kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, Mombasa, Kilifi, Lamu na Kwale pamoja na sehemu za pwani za Kaunti ya Tana River zilitarajiwa kupata mvua ndogo katika muda wa siku tano zijazo.

Tangazo hilo linajiri siku chache baada ya Mkurugenzi wa Kenya utabiri w Hali ya Hewa Kenya Dkt David Gikungu kuwataka Wakenya kujiandaa kwa mvua hadi Desemba.

Huku mvua kubwa ikitarajiwa kuendelea katika maeneo kadhaa nchini, idara ya hali ya hewa pia imewashauri Wakenya hasa wanaoishi katika kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi kuwa waangalifu.

Kulingana na idara, halijoto ya usiku katika kaunti zilizotajwa hapo juu inatarajiwa kushuka hadi nyusi 12°C kwa siku mbili za kwanza za utabiri kabla ya kushuka zaidi hadi 10°C kwa siku zilizosalia.

Zaidi ya hayo, idara ya hali ya hewa ilitangaza kuwa joto la juu wakati wa mchana litashuhudiwa katika kaunti za Kaskazini Mashariki za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Isiolo, Turkana na Samburu.

Halijoto ya mchana ilitarajiwa kupanda hadi nyusi 37°C kwa siku tatu za kwanza za utabiri wa hali ya hewa kabla ya kupungua hadi nyusi 35°C kwa siku zilizosalia.