Huenda Kalonzo akaachwa mataani handisheki ya Ruto na Uhuru ikiiva
HUENDA kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka akajipata mpweke kisiasa iwapo minong’ono kwamba Rais William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta wamezika tofauti zao na washirika wa rais huyo wa nne wanaelekea kujiunga na serikali ya Ruto.
Tangu Rais Ruto na Bw Kenyatta wahudhurie hafla ya kutawazwa kwa Askofu Paul Ndung’u wa Dayosisi Katoliki ya Embu wiki iliyopita, fununu zilichipuka kuwa wawili hao wamekuwa wakizungumza na huenda washirika wa Bw Kenyatta katika chama cha Jubilee ambao wamekuwa wakionekana na Bw Musyoka wakateuliwa katika nyadhifa za juu katika mabadiliko yanayotarajiwa serikalini baada ya Rigathi Gachagua kuondolewa ofisini.
“Handisheki ya Ruto na Uhuru iko njiani huku uteuzi ukitarajiwa kufanywa kufikia Ijumaa,” mdadisi wa siasa na mwanaharakati Ndung’u Wainaina aliandika kwenye X.
Washirika wa Kenyatta
Miongoni mwa majina ya washirika wa Bw Kenyatta wanaotajwa kujumuishwa katika serikali ni aliyekuwa gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi na katibu mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni na dadake Kenyatta, Bi Kristina Pratt.
Ingawa haikujulikana nyadhifa ambazo washirika wa rais huyo mstaafu wanaweza kutengewa, inasemekana ukuruba wake na Rais Ruto uliota baada ya Bw Gachagua kuondolewa ofisini.
Familia ya Kenyatta haikuwa na uhusiano mwema na Bw Gachagua ambaye inaamini alichochea jamii ya Mlimani dhidi yake na hasa uvamizi katika shamba la Northlands mwaka jana ambako mali ya mamilioni iliharibiwa na kuporwa.
Bw Gachagua aliomba msamaha familia ya Kenyatta lakini haikujulikana iwapo familia ya rais huyo wa zamani ilimsamehe.
Bw Musyoka amekuwa akimchangamkia Bw Gachagua ikisemekana ananuia kuungana naye kabla ya uchaguzi mkuu ujao huku akiongoza ‘mabaki’ ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.
Baada ya aliyekuwa mgombea urais wa muungano huo Raila Odinga kupatana na Rais Ruto na washirika wake kuteuliwa mawaziri, na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua aliyekuwa mgombea mwenza wa Raila kujitenga na Azimio, Wiper, Jubilee ya Bw Kenyatta, DAP-K ya Eugene Wamalwa na PNU ya Peter Munya ndio walibaki katika Azimio kuendeleza ajenda ya upinzani.
Bw Kioni , Bw Wamalwa na Bw Munya wamekuwa wakimtambua Bw Musyoka kama kiongozi wa Azimio baada ya ndoa ya kisiasa kati ya Rais Ruto na Bw Odinga kufanyika.
Mlima Kenya
Musyoka amekuwa akichangamkia eneo la Mlima Kenya baada ya uhusiano wa Ruto na Gachagua kutibuka huku ikisemekana muungano wa jamii za eneo hilo wa GEMA umepanuliwa kushirikisha jamii ya Wakamba.
Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa wanasema bila baraka za Bw Kenyatta, itakuwa vigumu kwa Musyoka kupenya eneo hilo kisiasa. Wanasema iwapo ukuruba unaodaiwa kati ya Ruto na Kenyatta utaota mizizi, Bw Musyoka ataachwa pweke katika siasa za Kenya.
“Ukuruba wa Ruto na Kenyatta utakuwa pigo kwa Musyoka ambaye tayari amempoteza Bw Odinga ambaye wamekuwa wakishirikiana kwa zaidi ya miaka 15. Isisahaulike kwamba Kenyatta ndiye mwenyekiti wa Azimio na akiondoa chama chake Muungano huo utakufa rasmi na kuacha Musyoka pabaya,” anasema mchambuzi wa siasa Ken Kasina.
Kwa mujibu wa mchambuzi huyu, hata Bw Musyoka akikubaliana na Bw Wamalwa hawawezi kuwa na nguvu kukabili ushirika wa Ruto, Kenyatta na Odinga katika uchunguzi wa 2027.
Kufikia sasa haijabainika iwapo Bw Kenyatta ana mkataba wowote wa maelewano na Rais Ruto. Hata hivyo, inasemekana kuwa Kenyatta analenga zaidi kulinda maslahi ya kibiashara kuliko kuokoa maisha ya kisiasa ya vigogo kama Musyoka.