Majaji 10 hatarini kutimuliwa kwa maamuzi tata katika kesi
MAAMUZI ya majaji kadhaa yaliyotambua agizo lililopingwa licha ya kutokuwa halali yanatishia kusimamisha shughuli za Mahakama ya Juu kufuatia ombi la kutaka majaji wake wanne kuondolewa madarakani.
Mwenyekiti wa Kituo cha Baraza la Utamaduni Kenya, Bw Kungu Muigai na aliyekuwa Mbunge wa Gatundu Ngengi Muigai wanataka majaji 10 watimuliwe kwa madai ya utovu wa nidhamu katika kushughulikia mzozo uliodumu kwa miongo kadhaa kuhusu shamba la ekari 443 huko Juja, Kaunti ya Kiambu.
Bw Kungu na kakake Bw Ngengi walipoteza ardhi yao ya ekari 443 kufuatia kesi kadhaa mahakamani dhidi ya Benki ya KCB na baadaye dhidi ya kampuni iliyonunua ardhi kupitia mnada 2007.
Hasara hiyo ilitokana na uwekezaji duni wa kilimo cha maua ambacho ndugu hao walijaribu mwaka wa 1989, wakitumia mashamba katika Kaunti za Nyandarua na Kiambu kama dhamana ya mkopo kutoka Benki ya KCB.
Bw Kungu ameitaka JSC kumwita atoe ushahidi, ikihitajika, kwani anataka tume hiyo kuanza mchakato wa kutimua majaji hao 10 ofisini.
Majaji 30 wa Mahakama Kuu
Mizozo kuhusu ardhi hiyo uliibua kesi 25, ambazo zimeshughulikiwa na zaidi ya majaji 30 katika Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu.
Ndugu hao wamewasilisha maombi yao kupitia Benjoh Amalgamated iliyopata mkopo mwaka wa 1989, na Muiri Coffee Estates, mdhamini aliyepoteza shamba hilo la ekari 443.
KCB iliuzia Bidii Kenya Ltd shamba hilo kwa Sh70 milioni mwaka wa 2007.
Ndugu hao wanateta katika ombi lao kuwa wakati wa mnada huo, ardhi hiyo ilikuwa na thamani ya Sh1.3 bilioni. Wanasema kwenye hati za kiapo kwamba mali hiyo sasa ina thamani ya zaidi ya Sh3 bilioni.
Mnunuzi huyo alimiliki ardhi hiyo mnamo Machi, 2024 baada ya kesi nyingi zinazohusiana na mali hiyo kuamuliwa kupendelea KCB na Bidii Kenya Ltd.
Kilimo cha maua
Mzozo huo ulitokana na mkopo wa Sh23 milioni uliokopwa na Benjoh Amalgamated mnamo 1988 kwa uwekezaji wa kilimo cha maua chini ya mradi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Amerika (USAID).
Benjoh Amalgamated ilitoa sehemu mbili za ardhi huko Nyandarua kama dhamana, huku Muiri Coffee Estate ikitoa ardhi ya Juja ya ekari 443 kama mdhamini zaidi.
Benjoh Amalgamated kwa miaka mingi imeshikilia kuwa KCB ilihujumu mipango yake kwa kukataa kutoa sehemu ya mkopo huo ambao ulinuiwa kuendeleza ukuzaji wa maua ya kuuza nje ya nchi.
Hii, kampuni ilisema, ilichangia kushindwa kulipa mkopo.
Benjoh iliishtaki KCB isitishe mnada uliopangwa mwaka wa 1992. Lakini faili ya mahakama ilitoweka kabla ya KCB kuwasilisha utetezi wake.
Mahakama Kuu ilipoamuru kuundwa upya kwa faili hiyo kupitia hati ambazo kila mhusika alikabidhiwa, KCB iliwasilisha amri iliyoiruhusu kupiga mnada shamba ikiwa Benjoh haingelipa mkopo huo ndani ya muda uliokubaliwa ambao ulikuwa umepita.
Ndugu hao wa Muigai wanashikilia kuwa KCB iliwasilisha nakala ambazo hazikuonyesha ni pesa ngapi zilikuwa zimelipwa kwa mkopo huo.
Benjoh alipinga hati hiyo, bila kufaulu.
KCB ilichagua kupuuza dhamana ya Benjoh na badala yake ikalenga ardhi ya mdhamini wa pili ya ekari 443.
Maagizo ya mahakama yalizuia mnada uliokuwa umepangwa hadi 2007 ambapo KCB hatimaye iliuzia Bidii Kenya.
Kushindwa kulipa mkopo
Maamuzi mengi yaliyoafikiwa na Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu yalitokana na agizo la mwaka wa 1992 ambalo lilionyesha kuwa KCB ilikuwa huru kupiga mnada shamba hilo iwapo Benjoh Amalgamated ilishindwa kulipa mkopo wa Sh23 milioni.
Kupitia ombi lililopokelewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama (JSC) mnamo Oktoba 11, 2024 Bw Muigai sasa amewashutumu majaji hao 10 kwa kuegemeza maamuzi yao mbalimbali kutokana na amri isiyo halali, ambayo anasema ilisaidia kupoteza mali yake kwa njia isiyo ya haki.
Ombi hilo linaweza kuhatarisha shughuli za Idara ya Mahakama kwa kuwa linataka kuondolewa kwa majaji wanne wa Mahakama ya Juu – zaidi ya nusu ya majaji wa mahakama hiyo ya upeo.
Ombi hilo pia linataka kuondolewa kwa majaji sita wa Mahakama ya Rufaa.
Bw Muigai katika stakabadhi zake anasema kwamba ombi la kuondolewa madarakani linaweza kuwa nafasi yake ya mwisho kupata haki, hata anapofichua kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inachunguza madai ya ulaji hongo kuhusiana na kesi kuhusu ardhi hiyo.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA