Kiongozi wa kanisa anayedaiwa kumdunga kisu mkewe mara 18 ajisalimisha kwa polisi
ELIAS Njeru Mutugi aliyedaiwa kumdunga kisu mpenzi wake mara 18 mjini Nakuru, amekamatwa baada ya kujisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Menengai akiandamana na wakili wake.
Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 35 alijisalimisha kwa polisi Jumatatu asubuhi.
Njeru alitoroka baada ya kumvamia mchumba wake, mfanyabiashara wa Nakuru Florence Wanjiku Gichohi, akamkata vidole vyake na kumwacha akiuguza majeraha ya visu.
Mwathiriwa anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Nakuru.
Kulingana na mkuu wa Polisi eneo la Bonde la Ufa Jasper Ombati, mshukiwa alitoroka eneo hilo baada ya kisa hicho cha Alhamisi hadi Jumatatu asubuhi alipojisalimisha kwa polisi, akiwa na wakili wake.
“Alijisalimisha kwa polisi Jumatatu asubuhi, akiwa na wakili wake Gakuhi Chege. Alikamatwa na huenda akakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua baada ya kudaiwa kumdunga mpenziwe Florence Wanjiku Gichohi kwa kisu kufuatia ghasia za kinyumbani nyumbani kwao Kiamunyi wiki jana,” akasema Bw Ombati.
Mshukiwa alimvamia mwathiriwa nje ya nyumba yake eneo la Kimunyi, baada ya kuomba kukutana naye miezi kadhaa baada ya kutengana.
Alikuwa ameomba wawili hao wakutane katika Hoteli ya Nakuru’ Alps ili kujadiliana kuhusu biashara waliyofanya pamoja kabla ya kutengana, lakini alimgeuka na kumshambulia.
Njeru ambaye mfanyabiashara na kiongozi mkuu katika kanisa moja mjini Nairobi, alimdunga kisu kichwani, mgongoni, mkononi na sehemu nyingine za mwili na kumwacha katika hali mbaya.
Bi Wanjiku sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Optimum katika jiji la Nakuru.
Kabla ya kutengana, wawili hao walikuwa wakiendesha kampuni ya kununua na kuuza ardhi na mali, ambayo ina ofisi katika Jengo la CK Patel katikati mwa Jiji la Nakuru.
Wapenzi hao wawili wa zamani pia walikuwa na watoto wawili pamoja.
Mnamo Jumamosi, baadhi ya viongozi wanawake wakiongozwa na Katibu wa Jinsia na Huduma za Kijamii Anne Wang’ombe waliomtembelea mwathiriwa hospitalini walilaani shambulio hilo wakitaka haki itendeke haraka.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA