Habari za Kitaifa

Uozo Kaunti ya Laikipia Bodi ya Mapato ikiitisha ngono na hongo kujaza nafasi 250 za ajira

Na MWANGI NDIRANGU November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BODI ya Ukusanyaji Ushuru ya Kaunti ya Laikipia imemulikwa baada ya baadhi ya maafisa kuhusishwa na madai ya ngono na rushwa kutoka kwa watu wanaosaka ajira katika idara ya kukusanya ushuru.

Wahasiriwa wa sakata hii wamedai pia kuwa wanaagizwa kulipa Sh80,000 ili kupata nafasi chache zilizopo za ajira.

Hata baada ya kutimiza masharti hayo, waliachwa nje ya orodha ya mwisho iliyotangazwa mwezi uliopita.

Bodi hiyo Septemba ilitangaza nafasi 250 za ajira baada ya muda wa kandarasi za mwaka mmoja za wafanyakazi walioajiriwa Oktoba mwaka uliopita, kukamilika.

Baadhi ya wafanyakazi ambao kandarasi zao zilikamilika Oktoba 31 walipaswa kuruhusiwa kuendelea na kazi na walilengwa kirahisi kupitia kuitishwa ngono na hongo.

Watu karibu 4,000 waliwasilisha maombi yao kwa nyadhifa chache zilizosalia na kusababisha visa tele vya ukora kupitia kwa watu maarufu katika serikali hiyo ya kaunti ikiwemo wanachama wa bodi ya mapato, mawaziri, maafisa wakuu, madiwani, na watu binafsi walio karibu na Gavana Joshua Irungu.

Suala hilo sasa limefika katika Bunge la Kaunti ya Laikipia ambapo hoja ya kuvunjilia mbali kwa bodi hiyo imewasilishwa.

Kamati ya Leba, Maslahi na Huduma kwa Jamii iliwasiliana na wahasiriwa wa sakata za ngono na rushwa na kuandaa ripoti itakayowasilishwa mbele ya bunge la kaunti, Oktoba 26, 2024.

“Ili kuangamiza ufisadi katika kaunti ya Laikipia, bodi yote inapaswa kuvunjwa. Ili kupigana na dhuluma za kingono zinazowalenga watu wasiokuwa na hatia wanaosaka kazi, bodi yote inastahili kwenda nyumbani,” Diwani wa Wadi ya Thingithu, Stephen Ndiritu, alisema alipowasilisha hoja Ijumaa.

Diwani mteule, Leila Hussein alisema hata ikiwa ni mwanachama mmoja tu wa bodi anayehusika na maovu hayo, itakuwa haki iwapo bodi yote itavunjwa ili kulinda uadilifu wa taasisi hiyo.

“Inasikitisha kuwa katika enzi hii, watu maarufu serikalini wananyemelea wasichana wachanga kwa kuitisha kujamiiana kwa sababu ya kandarasi ya mwaka mmoja yenye mshahara ulio chini ya Sh20,000. Wahusika hawa hawapaswi kusitiriwa. Ni sharti wakabiliwe bila huruma,” alisema Bi Hussein akirai bunge la kaunti kuwahakikisha ulinzi wanaotoa ushahidi mbele ya kamati.

Bodi ya mapato ina wanawake watatu na wanaume wanne akiwemo mkurugenzi.

Kwa sasa haina mwenyekiti baada ya aliyekuwapo kujiunga na Bodi ya Watumishi wa Umma.

Waliofanikiwa kuajiriwa walitazamiwa kuanza kazi Novemba 1, 2024 na tayari walikuwa wamehudhuria kozi ya siku moja ya mafunzo mjini Nyahururu lakini mchakato huo ulisogeshwa hadi mapema Disemba kufuatia madai ya ufisadi na mchakato wote kuingiliwa.

IMETAFSIRIWA NA MARY WANGARI