Habari za Kitaifa

Kiongozi wa kanisa aliyedunga kisu mpenziwe ashtakiwa kwa kujaribu kuua

Na  JOHN NJOROGE November 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ELIAS Njeru Mutugi, 35, mwanamume anayelaumiwa kwa kumdunga kisu mpenzi wake mara 18 mjini Nakuru, Jumatatu alasiri alifikishwa katika Mahakama ya Molo.

Njeru, ambaye ni kiongozi wa kanisa moja Nairobi, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Daisy Mose alishtakiwa kwa jaribio la kuua.

Mahakama ilimwachilia Njeru kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au Sh200,000 pesa taslimu.

Mahakama iliambiwa kwamba akiwa na silaha hatari, mshtakiwa alijaribu kinyume cha sheria, kusababisha kifo cha Florence Wanjiku Gichohi huko Kiamunyi, Rongai, kaunti ya Nakuru kwa kumdunga kisu mwili mzima na kumkata vidole, kosa alilotenda mnamo Novemba 21.

Elias Njeru akisikiza mashtaka kortini Molo. Picha|John Njoroge

Haya yalijiri saa chache baada ya Njeru kujisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Menengai akiandamana na wakili wake Gakuhi Chege.

Polisi walisema Njeru alitoroka baada ya kudaiwa kumvamia Bi Wanjiku, mpenziwe ambaye walikuwa wameachana.

“Alijisalimisha kwa polisi Jumatatu asubuhi, akiwa na wakili wake Gakuhi Chege.

Alikamatwa na atakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua baada ya kudaiwa kumdunga mpenziwe Florence Wanjiku Gichohi kwa kisu kufuatia ghasia za kinyumbani nyumbani kwao Kiamunyi wiki jana,”  mkuu wa polisi eneo la Bonde la Ufa Jasper Bw Ombati alisema Njeru alipojisalimisha.

Wakili wake Gakuhi Chege aliomba mahakama imwachilie mteja wake kwa dhamana akisema, kwa kuwa alijisalimisha kwa polisi, hakuwa hatarini kutoroka.

Elias amekanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000. Picha|John Njoroge

Mahakama ilikubali ombi la Njeru la kuachiliwa kwa dhamana.

“Hakuna sababu yoyote iliyotolewa na upande wa mashtaka kuilazimisha mahakama hii kumnyima mshtakiwa dhamana. Mahakama hii inamwachilia kwa dhamana ya Sh500,000 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho au dhamana ya fedha taslimu Sh200,000,” hakimu alisema.

Hata hivyo, mahakama iliamuru mshtakiwa asiingilie uchunguzi unaoendelea.

“Mahakama inaagiza  mshtakiwa asijaribu kuingilia uchunguzi unaoendelea na hapaswi kukanyaga Kiamunyi ambapo uhalifu ulifanyika au kwenda karibu na malalamishu au nyumba yake,”  hakimu aliagiza.

Kesi hiyo itatajwa Disemba 9, 2024.