Gachagua asema amepokonywa walinzi kabisa ‘baada ya Ruto kuzomewa Embu’
ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amefichua kuwa serikali sasa imewaondoa kabisa walinzi wake ikimlaumu kwa kufadhili upinzani dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.
Haya yanajiri huku duru katika Wizara ya Masuala ya Ndani zikiambia Taifa Leo kwamba ‘wenye ushawishi katika nchi hii wanataka Bw Gachagua azuiwe kuingiza nchi katika hali ya kampeni za mapema ili kuwezesha serikali kutekeleza miradi ya maendeleo’.
Duru hizo ziliongeza kuwa Bw Gachagua anaonekana kuwa na nia ya kuongoza uasi dhidi ya serikali hivyo basi ni lazima azuiwe.
“Hapa tuna mtu tuliyemshauri kwa busara ajiuzulu badala ya kungoja kutimuliwa.”
“Tulikuwa tumemhakikishia kuwa atahifadhi walinzi, bajeti, marupurupu na kuendelea na mpango wa kufufua siasa kabla ya 2027,” afisa katika wizara hiyo alisema kwa sharti asitajwe jina.
Nafasi ya kuzuru nchini
Aliongeza, “Wakubwa wetu kutoka afisi kuu wametuelekeza kumshughulikia Bw Gachagua kwa njia isiyompa nafasi ya kuzurura nchini.”
Bw Gachagua, Jumatatu kupitia kwa katibu wake wa kibinafsi Bw Munene wa Mumbi aliambia Taifa Leo kuwa matatizo yalianza baada ya Rais Ruto kuzomewa katika kanisa Katoliki la Embu.
“Kisha kilifuata kisa cha Ijumaa iliyopita katika Kaunti ya Murang’a ambapo wakati wa hafla ya mazishi ya aliyekuwa MCA maalum, Bw Mark Wainaina, waombolezaji walikataa rambirambi za Rais na Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki kusomwa,” Bw Mumbi alisema.
Bw Gachagua hakuhudhuria hafla ya mazishi Murang’a. Aliongeza kuwa Bw Gachagua alipozuru Murang’a Jumapili kwa ibada katika kanisa la Kangari AIPCA, walinzi wawili waliosalia waliondolewa.
“Ni kweli tunapozungumza Bw Gachagua hana hata afisa mmoja wa usalama wa serikali. Tulipouliza kutoka kwa afisi za serikali, tuliambiwa Bw Gachagua lazima akome shughuli za kisiasa,” Bw Mumbi alijibu.
Zaidi ya maafisa 200 wa usalama wa Bw Gachagua waliondolewa mara moja, Seneti ilipothibitisha kuondolewa kwake kama naibu wa rais na Bunge la Kitaifa mnamo Oktoba 17, 2024.
Nyumba zake mbili Nairobi na Nyeri
Maafisa hao walikuwa wakilinda nyumba zake mbili za Nairobi na mashambani Nyeri pamoja Aidha, maafisa waliohusika kumlinda moja kwa moja waliondolewa alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Karen baada ya kuugua ghafla.
Bw Mumbi alisema ufichuzi wa Bw Gachagua ulifanya serikali kuwarejesha maafisa wanne wa usalama kumlinda.
“Maafisa hao wanne kutoka Kitengo cha Kukabiliana na Fujo (GSU) baadaye waliondolewa na nafasi yao ikachukuliwa na maafisa wanne wa Polisi wa Utawala,” Bw Mumbi alisema.
Aliongeza kuwa waumini walipomzomea rais huko Embu, maafisa hao wanne waliondolewa jioni.Bw Gachagua alihudhuria hafla hiyo ya kanisa pamoja na rais Ruto lakini alivutia umati uliomshangilia tofauti na rais.
“Serikali ilimpa Bw Gachagua walinzi wawili baadaye alipolalamika alikuwa akiandamwa na watu alioshuku walikuwa na magari yenye nambari za kutiliwa shaka. Lakini baada ya naibu rais huyo wa zamani kuzuru Kaunti ya Murang’a Jumapili na kupokelewa vyema na wakazi, maafisa hao wawili waliondolewa,” alisema.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA