Washirika wa Rais wazomea maaskofu waliokataa michango, wachomoa mihela zaidi
WASHIRIKA wa karibu wa Rais William Ruto – Farouk Kibet na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah – wameonekana kuwasuta maaskofu wanaokataa michango huku wakizidi kutoa mamilioni na kuapa kuendelea kutoa.
Wawili hao walitoa Sh5 milioni katika kanisa Kaunti ya Pokot Magharibi, ambapo waliwasuta baadhi ya viongozi wa kidini wakidai walikuwa wakiwatusi wanasiasa.
Michango yao katika Kanisa la AIC Kitalaposho Jumapili ilijumuisha Sh2 milioni kutoka kwa Rais Ruto, Sh1 milioni kutoka kwa naibu wake Kithure Kindiki na Sh1 milioni kutoka kwa Bw Kibet na Bw Ichung’wah.
Bw Kibet na Ichung’wah, ambao walisema walimwakilisha Rais Ruto kwenye harambee ya kuchangisha pesa kanisani humo, walitangaza kwamba wataendelea kuchangia makanisa licha ya kukosolewa, wakisema kuwa ni kwa kazi ya Mungu wala si ya viongozi wa kidini.
Washirika wa Rais walisema makanisa hayawezi kujengwa bila michango.
“Hatuibi pesa ili kutoa michango. Tunatoa pesa hadharani na si sawa kutuhukumu sisi tunaofanya hivyo. Si kwamba tuna pesa nyingi za kutoa,” alijitetea Bw Kibet.
Hata baada ya maaskofu kukataa michango ya wanasiasa waziwazi juma moja lililopita, wanasiasa wameongeza kejeli na kujigamba kuwa wataendelea kutoa, watu wapende wasipende.
“Hatutoi pesa kanisani ili kuwafurahisha maaskofu. Hatuwezi kukoma kutoa pesa kwa makanisa,” alijipiga kifua Bw Ichung’wah akikashifu viongozi wa kidini huku akiwatuhumu kwa kuwalaumu wanasiasa.
Mnamo Novemba 17, katika Kanisa Katoliki la Soweto jijini Nairobi, Askofu Mkuu wa Katoliki wa Nairobi alikataa mchango wa Sh2.8 milioni uliotolewa kwa kanisa hilo.
Rais Ruto alitoa Sh 2.2 milioni za ujenzi wa nyumba ya padre na Sh600,000 kwa kwaya ya kanisa.
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alitoa Sh200,000. Rais aliahidi kutoa Sh3 milioni zaidi kusaidia katika ujenzi wa nyumba ya kasisi na kununulia kanisa basi lakini Askofu Mkuu Kasisi Philip Anyolo alikataa michango hiyo na kusema pesa zilizotolewa zitarudishwa.
Akiwa Pokot Magharibi, Bw Ichung’wah na Bw Kibet walidai viongozi wa kanisa hawakurudisha pesa hizo.
“Wakizirudisha, nitachukua pesa hizo na kuzileta hapa Pokot Magharibi ambako watu wengi wanazihitaji,” Bw Kibet alisema na kuongeza hakuelewa sababu ya ‘baadhi ya watu kupinga michango.’
Bw Kibet alisema wachungaji wanafanya makosa akidai wanapinga miradi ya maendeleo kwa Wakenya.
“Ili kukamilisha miradi hii, wanahitaji michango. Maaskofu wanapaswa kujua kuwa wao ni Wakenya kama sisi. Hawafai kujiona wakiwa wakubwa wanapovaa vikosi vyeupe na kutuhujumu,” Bw Kibet akasema akidai viongozi wa kidini wanawatukana viongozi.
“Sifai kuambiwa eti nisitoe mchango. Ninatoa pesa kwa Mungu. Tumekuja hapa kutoa pesa ya kusaidia katika ujenzi wa kanisa,” akaongeza.
Akiwa waziri wa usalama wa ndani, Prof Kindiki hakuonekana akimwaga pesa nyingi hadharani kama inavyoshuhudiwa sasa baada ya kuchukua wadhifa wa Naibu Rais mnamo Novemba 1.