Habari za Kitaifa

Dili zilizofutwa Kenya hazingenisaidia kwa kitu, Adani sasa asema

Na  JOHN MUTUA November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI ya Adani Group kutoka India, imepuuza athari za uamuzi wa Kenya wa kufuta kandarasi yake ya kujenga laini za kusambaza umeme na vituo vidogo vya stima ikisema hauathiri mapato yake hata kidogo.

Kampuni hiyo ya India, ambayo ingenufaika na Sh637.7 bilioni kutokana na mkataba huo, ilisema kuwa kufutwa kwa kandarasi hizo sio kitu kwake.

Kampuni hiyo ilitarajiwa kupata Sh637.7 bilioni katika kipindi cha miaka 30 au wastani wa Sh21.23 bilioni kwa mwaka kupitia mradi wa ujenzi wa laini za kusambaza umeme kwa kima cha Sh95 bilioni ambazo ingesimamia.

Sh21.23 bilioni zinawakilisha asilimia 0.004 ya Sh4.78 trilioni ambazo Adani Group ilitarajia kama mapato kwa mwaka hadi Machi, na imetaja hasara yoyote kufuatia kufutwa kwa kandarasi hiyo kama isiyoweza kuathiri biashara yake kwa vyovyote.

Ilisema  hayo  ikijibu ombi la ufafanuzi kutoka kwa Soko la Hisa la Bombay na Soko la Hisa la Kitaifa baada ya Rais William Ruto kuamuru kufutwa kwa ushirikiano wa miaka 30 wa kampuni hiyo kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi (PPP).

Mnamo Alhamisi Novemba 21, Rais Ruto pia aliamuru kufutwa kwa mchakato wa ununuzi ambao ulikuwa unatarajiwa kutoa udhibiti wa uwanja mkuu wa ndege wa Kenya (JKIA) kwa Adani Group ya India.

Hii ilikuwa ni siku moja baada ya Amerika kumfungulia mashtaka mwanzilishi wa Kundi la Adani, Gautam Adani na watu wengine saba, kwa madai  walilipa Sh34.3 bilioni kama hongo kwa maafisa wa India. Ufichuzi wa Amerika ulisababisha Kenya kuchukua hatua.

Kundi hilo lilikanusha madai ya Amerika, na kusema ” hayana msingi.” Hata hivyo, hatua hiyo tayari inaumiza kampuni hiyo na uchumi wa India. Kampuni za Adani Group zilipoteza thamani ya soko ya dola 39 bilioni baada ya wakuu wake kufunguliwa mashtaka Amerika, na kupunguza mtaji wa soko wa kampuni zake 10 hadi dola 142.6 bilioni (Sh18.45 trilioni).

Ilitaja kufutwa kwa mikataba yake Kenya kama hatua isiyo na maana, ikisisitiza utajiri wa Gautam na ukubwa wa kampuni ya Adani Group—ambao mapato  ni zaidi ya mara 14 yale ya Safaricom, kampuni tajiri zaidi Afrika Mashariki inayotangaza mauzo ya kila mwaka ya Sh335.3 bilioni.

Kwa thamani yake ya Sh18.45 trilioni, thamani ya soko ya Adani Group ni kubwa kuliko makadirio ya jumla ya pato la Kenya la Sh13.9 trilioni. Kampuni hiyo ilitarajiwa kupata faida kubwa kwa miaka 30 kabla ya kukabidhi laini za kusambaza umeme kwa serikali ya Kenya.