Habari za Kitaifa

Mahakama kuu yakataa kuzuia ubomoaji wa majumba mtaa wa Woodley

Na RICHARD MUNGUTI November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

WAKAZI wa moja ya mitaa mikongwe zaidi jijini Nairobi ya Woodley na Joseph Kang’ethe wamepoteza azma yao ya kuzuia serikali ya Gavana Johnson Sakaja kuwafukuza na kuwabomolea majumba yao ambayo wameishi miaka 60 sasa.

Kuangushwa kwa majumba haya na matingatinga ya mwekezaji Africa Reit Limited yameibua jinsi mwanaharakati Charles Yaw Sosah alipouawa miaka 23 iliyopita kwa kupinga unyakuzi na ubomolewaji wa majumba hayo yaliyo makazi ya watu wa tabaka mbali mbali.

Sosah aliandamwa na wanaume wawili waliokuwa wamejihami kwa bastola na wakammiminia risasi 16.

Wakili mwenye tajriba ya juu Dkt John Khaminwa aliyewakilisha wakazi zaidi ya 40 ambao majumba yao yalibomolewa alimweleza Jaji Oguttu Mboya “makazi haya ya Woodley na James Kang’ethe yana kumbukumbu kali za historia ndefu ya nchini hii iliyowaunganisha watu wa tabaka mbali punde tu nchi hii ilipojinyakulia uhuru.”

“Gavana Muingereza wa mwisho kutawala nchi hii pamoja na aliyekuwa Meya wa Nairobi waliwapa watu wa tabaka mbali mbali — Waafrika, Wazungu na Wahindi — makazi katika mitaa hii ili kufutilia mbali kasumba na hisia za ukoloni,” Dkt Khaminwa alimweleza Jaji Oguttu Mboya na kumsihi azime Serikali za kaunti ya Nairobi na Serikali Kuu kubomoa majumba katika mtaa huo.

Sosah aliyekuwa na umri wa miaka 34 alipouawa mnamo Feburuari 11, 2001 alikuwa mtetezi shupavu wa mitaa hiyo ya Woodley na James Kang’ethe.

Mtutu wa bunduki

Sosah aliangushwa kwa mitutu ya bunduki na waahini waliokuwa wanamezea mate kunyakua mitaa hiyo.

Wauaji wa Sosah walitoweka hadi waleo, polisi wangali wanawasaka.

Lakini aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango katika Baraza la Mji wa Nairobi (NCC) Kuria wa Gathoni alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya Sosah.

Wa Gathoni aliachiliwa na Mahakama kuu kisha akaishtaki serikali kwa kumfungulia mashtaka kimakosa na akafidiwa Sh26 milioni.

Tangu mauaji ya Sosah, wakazi wa Woodley waliunda chama almaarufu Woodley Estate Residents Welfare Society (WERWS) kulinda na kuzuia unyakuzi wa mtaa wao.

Katika kesi iliyoshtakiwa na wakazi wawili Joseph Ngotho na Pinto Kali kwa niaba ya wakazi wengine 41, Dkt Khaminwa alimsihi Jaji Oguttu Mboya azime hatua ya kubomoa majumba hayo ya Woodley na Joseph Kang’ethe.

Lakini Jaji Mboya alitupilia mbali kesi hiyo ya wakazi hao wa Woodley.

Akitupilia mbali ombi la wakazi hao Jaji Oguttu Mboya alisema “walalamishi hawakujitambulisha kwa majina katika kesi hiyo ndipo mahakama ijue inahusika na nani.”

Wakazi wawili Joseph Ngotho na Pinto Kali ndio waliojitambua katika kesi waliyoshtaki kwa niaba ya wakazi wengine 41 wa mitaa ya Woodley na Joseph Kang’ethe jijini Nairobi.

Katika uamuzi wa kurasa 42, Jaji Mboya alisema wakazi hao wameficha majina yao na itakuwa vigumu kujua wakazi halisi na wale wa kujipendekeza.

Jaji huyo alikubalia ombi la wakili Dkt Adrian Kamotho kwamba “kesi hiyo inafaa kutupwa tu kwa vile walalamishi halisi hawajulikani.”

Pia mahakama ilielezwa wakazi hao wameshindwa kuthibitisha malalamishi yao ipasavyo.

Kubomolewa kwa majumba hayo ya mitaa ya Woodley na James Kang’ethe kumezua taharuki miongoni mwa wakazi na wakitilia shaka uhalali wake.

Hisia kali za wakazi wa Woodley

Hakimu alielezwa kwamba matukio ya hapo awali yanasababisha hisia kali na kuona kwamba serikali haitaki kulinda maslahi ya wakazi hawa.

Dkt Khaminwa alisema wakazi hawa hawajui mahala pengine wanapoweza kuita nyumbani.

Katika kesi hiyo, Mabw Joseph Ngotho, Pinto Kali na watu wengine 41 waliishtaki seriakali ya kaunti ya Nairobi, Mwanasheria mkuu na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC).

Kampuni ya uwekezaji ya Africa Reit Ltd (ARL) na chama cha wanasheria nchini (LSK) zilishtakiwa pia.

Jaji Mboya alitupilia mbali kesi ya wakazi hao akisema ubomozi tayari umefanyika na kwamba “kile mahakama ingelizuia kisifanyike kimefanyika tayari.”

Jaji huyo pia alisema wakazi hao hawakujitambua kwa majina na kwamba ni vigumu kujua walalamishi halisi.

Mahakama ilisema kesi hiyo ikisikizwa itatathmini ikiwa walalamishi watalipwa fidia au la.

Pia Dkt Khaminwa alisema atakata rufaa.