Muziki wa Bongo Flava wagawanya wazee Lamu
WAZEE kisiwani Lamu wametofautiana kuhusu iwapo ni sawa muziki wa Bongo Flava kuchezwa wakati wa maadhimisho ya kila mwaka ya Tamasha za Utamaduni wa Lamu.
Kila mwaka, waandalizi wa tamasha hizo huwaalika wasanii wa Bongo Flava kutoka Tanzania kutumbuiza watu wanaohudhuria hafla hiyo.
Mwaka huu, tamasha hizo zimepangiwa kufanyika kisiwani Lamu kuanzia Alhamisi, Novemba 28 hadi Jumamosi, Novemba 30.
Waandalizi tayari wametangaza kuwaalika wasanii kadha wa Bongo Flava, ikiwemo Dennis Mwasele, almaarufu kama D Voice na Bi Yasirun Yassin Shabaan, almaarufu kama Yammi.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo, baadhi ya wazee walilalamika kuwa, mara nyingi wasanii wa muziki wa Bongo Flava wanapotumbuiza hadhira wakati wa tamasha za utamaduni wa Lamu, wao huishia kwenda kinyume na azma ya sherehe yenyewe.
Dhamira kuu ya tamasha hizo huwa ni kuzienzi mila na tamaduni za Waswahili wa asili ya Wabajuni wapatikanao Lamu.
Bw Abdalla Faraj, mzee wa kisiwani Lamu, alisema ni mwiko kuwaona wanawake kwa wanaume wakisakata densi na kupapasana jukwaani wakati wasanii hao wanapotumbuiza hadhira.
“Utapata wasanii hawa wa Bongo Flava punde wanapoanza kutumbuiza, hadhira hushikwa na mihemko kiasi cha kuzisahau kabisa mila, itikadi na tamaduni za Lamu,” akasema Bw Faraj.
Kauli hii iliungwa mkono na Bw Ahmed Hussein, mkazi wa Lamu aliyesema kinachostahili kufanywa na waandalizi ni kupeana kipaumbele burudani zinazoendana na maudhui ya sherehe.
Densi asilia za Lamu kama Goma
Bw Hussein alisema ni vyema densi asilia za Lamu kama vile Goma, Chama, Kirumbizi, Uta, Thwari la Ndhiya, Lele Mama, Vugo, na nyinginezo kuchezwa wakati wa Tamasha za Utamaduni wa Lamu ili kuwawezesha wanaohudhuria hafla hiyo kujielimisha na tamaduni hizo za wenyeji wa Lamu.
“Maonyesho ya Tamasha za Utamaduni wa Lamu yanafaa kuwa yenye uasilia wa mila zetu. Wanaokuja Lamu kuhudhuria sherehe wanatazamia kujihamasisha kwa mengi ya zamani na ya sasa yanayoihusu jamii ya Lamu. Sidhani kuwaleta wasanii wa Bongo Flava kutoka Tanzania kunaafikiana na matarajio na maudhui ya sherehe husika,” akasema Bw Hussein.
Waziri wa Utamaduni Lamu, Bi Aisha Miraj alisema wasanii wote walioalikwa kutumbuiza kwenye sherehe za utamaduni wa Lamu hawataenda kinyume na yanayotarajiwa.
“Watu wasiwe na shaka. Hawa wasanii tumekutana nao tayari na kuwajulisha ni lipi hasa wanafaa kufanya wakati wanapotumbuiza jukwaani. Tumewashauri ikiwezekana hata wavae mavazi yanayodhihirisha tamaduni za Lamu,” akasema Bi Miraj.
Hata hivyo, wazee wengine walishikilia msimamo kwamba, tamasha hizo huvutia aina mbalimbali za watu kwa hivyo hakuna tatizo ikiwa baadhi ya wanaohudhuria wanapenda kutumbuizwa kwa muziki aina hiyo.
Bw Mohamed Hussein Noor, alisema ni wazi waandalizi huwa wanafuata kile wanachoona kinawapendeza wakazi na wageni wanaohudhuria tamasha hizo za utamaduni.
Alieleza kuwa, imekuwa wazi wakati maonyesho ya nyimbo za kiasili yanapoandaliwa ikiwemo Qasida, mashairi ya Kiamu, Kirumbizi, Goma la Lamu na kadhalika ni watu wachache hujitokeza.
Mwanzilishi wa Tamasha za Utamaduni Lamu, Bw Ghalib Alwy, alisema si vibaya kukaribisha wasanii wa Bongo Flava na wengineo kuzitia nakshi tamasha hizo.
“Si wasanii wa Tanzania pekee. Hata wale wa kutoka Misri, Morocco, Oman na kwingineko tumewaalika Lamu mara nyingi wakati wa maadhimisho ya tamasha zetu,” akasema Bw Alwy.