MAONI: Gachagua hakukemea maovu akiwa afisini, sasa afaa afyate mdomo
MATAMSHI ya aliyekuwa naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu kile kinachotajwa na wajuzi kuwa sakata ya Adani yanaibua shaka kuhusu maadili yake.
Yapo maswali yanayonijia akilini: Je, endapo angesalia kuwa naibu wa Rais William Ruto angeyasema haya?
Na je, anayasema haya kwa hiari ama ni vitisho kwa utawala wa Rais Ruto ambao unaonekana kunyong’onyea kwa hali zote? Tatu ikiwa angenyamazia suala hilo jinsi alivyofanya akiwa na kiti kikubwa serikalini, hatima yake kisiasa ingebadilika?
Kwa mtazamo wangu, hizo habari zilikuwa muhimu sana kwa Wakenya ikiwa zingetoka kwa mtu mwenye nia njema wala si jambo la masilahi.
SOMA PIA: MAONI: Ruto si Zakayo, wa Biblia alikuwa msikiza ushauri
Nilimsikiza Gachagua akisema ikiwa angekubaliana na miradi ya Adani hangefukuzwa kazi. Akasema ni yeye pekee katika baraza la mawaziri wa Rais Ruto ambaye alikuwa na ubavu wa kumkosoa.
Eti mawaziri wengine walikaa kimya kama maji ya mtungi, Rais akikodoa macho kila mtu anainama kwa hofu kubwa. Tunaweza kumwamini kwa hoja hiyo kwa sababu hatukai ikulu.
Matamshi ya Gachagua hayawezi kupuuzwa hata hivyo.
Lakini Je, tumwamini nani kati yake na Nelson Amenya aliyeifichua sakata hiyo? Amenya alitambua mikataba hii baada kukutana na stakabadhi zilizokuwa zikionyesha michoro ya wakubwa wa Kenya na Adani, kuu zaidi ikiwa ni kutwaa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Na muda si mrefu, habari za uwezekaji katika sekta ya kawi zikaibuka. Mawaziri Davis Chirchir na Opiyo Wandayi wakasema kuwa Adani yu sahihi.
SOMA PIA: KINAYA: Ikiwa miaka miwili ya utawala huu inachosha, si saba itaua?
Vyombo vya habari vinatakiwa kuchukua tahadhari kubwa kwa matamshi haya, siyo kukubali kimahubiri kila anachosema.
Pili, tunastahili kuchunguza haya matamshi yanalenga hadhira gani na yanasemwa katika majukwaa gani. Kwangu naona Gachagua amefaulu kushawishi sehemu ya Mlima kupitia kwa hoja ya Adani kuwa alionewa kwa kuwa msema kweli.
Mlimani baadhi ya sehemu hewa ya siasa imechafuka na wapinzani wa Gachagua wanaanza kujifikiria. Baadhi ya watu wanadhania yeye ni kiongozi wa taifa.
Gachagua amesema atatangaza msimamo wake mapema mwaka ujao. Wakenya wanasubiri. Ila mbunge huyo wa zamani anatakiwa achukue tahadhari kabla ya hatari ya siasa kummeza.
SOMA PIA: Ruto: Nilijumuisha Azimio kwenye serikali ili sote tuitwe Zakayo
Kwanza, anatakiwa abadili mkondo wa kusema mambo ya kitaifa nje ya eneo la kati ili kujenga sura ya taifa. Vinginevyo, atachukuliwa na sehemu kubwa ya Kenya kuwa kiongozi wa kikabila.
Haya ya kutengwa na mkubwa wake yalifanywa pia na watangulizi wake. Kwa mfano, Ruto alipodhania kuwa Rais Uhuru hakutaka amrithi, alikimbilia eneo la kati kuwalilia watu wa Mlima. Gachagua atafute utaifa kwanza.
Mwandishi ni Mhariri wa NTV