Korti yataka ushahidi kwamba Ruto alifuta dili za Adani
MAHAKAMA Kuu imeitaka serikali kuwasilisha ushahidi kuhusu kufutiliwa au kuondolewa kwa zabuni mbili za mabilioni ya fedha na kampun ya Adani Group, alivyotangaza Rais William Ruto wiki jana.
Dkt Ruto alitoa agizo hilo Alhamisi wakati wa hotuba yake kuhusu Hali ya Kitaifa mbele ya kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti.
Rais aliagiza kutamatishwa kwa zabuni ya ukarabati wa Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na ujenzi wa nyaya za kusambaza umeme ambazo zilikuwa zimepewa kampuni tanzu za Adani Group yenye asili yake nchini India.
Lakini walipofika mbele ya Jaji Bahati Mwamuye, walalamishi kupitia mawakili Kalonzo Musyoka na Kibe Mungai walisema hamna ushahidi mikataba hiyo imefutiliwa mbali.
“Tunachukulia taarifa hiyo kama geni hadi ushahidi wa kuithibitisha utawasilishwa,” Bw Musyoka akasema.
Aliongeza kwa walalamishi wataendelea na kesi hiyo hata baada ya serikali kuwasilisha ushahidi kuhusu kufutiliwa kwa zabuni zilizopewa Adani.
Ushahidi wa zabuni kuondolewa
“Washtakiwa watahitajika, katika majibu ya kesi hii, kutoa ushahidi wa kuonyesha kuwa zabuni hizo zilifutiliwa au kuondolewa,” akasema Jaji Mwamuye.
Aidha, Jaji huyo alitoa agizo linalozuia serikali kuweka mkataba kuhusu ukarabati na kupanuliwa kwa uwanja wa JKIA hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa. Kesi imewasilishwa na Tony Gachoka na walalamishi wengine.
“Agizo linatolewa kuzuia washtakiwa kuweka makubaliano na mshtakiwa wa kwanza na wa pili (Adani Group) au asasi zingine zinazohusiana nayo,” Jaji huyo akasema.
Mahakama hiyo iliamuru kesi hiyo itajwe mnamo Januari 29, ili maagizo zaidi yatolewe.
Hili ni agizo la pili la mahakama la kuzuia mkataba na Adani, baada ya jaji mwingine kutoa agizo kama hilo Septemba mwaka huu katika kesi iliyowasilishwa na Chama cha Mawakili Nchini (LSK) na Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC).
Rais Ruto alitangaza kufutiliwa mbali kwa mikataba ya Adani baada ya mmiliki wake bilionea Gautam Adani na watu wengine saba kushtakiwa nchini Amerika kwa tuhuma za ufisadi na ulaghai.
Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mahakama, inadaiwa kuwa Adani na wenzake walipanga njama ya kudanganya wawekezaji nchini Amerika kuhusu rekodi yake kuhusu utoaji hongo.
Taasisi za kimataifa za kifedha
Aidha, inadaiwa walihadaa taasisi za kimataifa za kifedha.
Vile vile, Adani na wenzake wanalaumiwa kwa kudanganya kuwa walijaribu kuhonga maafisa wa serikali ya India ili kupata faida ya mabilioni ya dola baada ya kupata zabuni ya kuuza vifaa vya kawi ya jua.
Ilisemekana kuwa mnamo 2022, Adani na maafisa wa kampuni zake, walipanga njama ya kutoa hongo kwa maafisa wa serikali ya kampuni ya usambazaji kawi nchini India ili wapate zabuni.
Shirika la Ujasusi la Amerika (FBI) lilisema kuwa watuhumiwa walitoa habari za uwongo kwa serikali ya Amerika wakati wa uchunguzi.