Makala

Mpango wa Ruto wa nyumba nafuu ulivyogeuka machozi kwa walipa ushuru, wakazi na wanakandarasi

Na WAANDISHI WETU November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MPANGO wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambao ulianzishwa na serikali ya Kenya Kwanza umebadilika kuwa machozi sio tu kwa wanaobebeshwa mzigo wa ushuru, wanaobomolewa makazi yao bali pia kwa wanakandarasi.

Serikali za kaunti zinazolenga kujenga nyumba za bei nafuu zimeungana na serikali kuu kubomoa makazi katika mitaa ambayo wakazi wamekuwa wakiishi kwa miaka mingi na kusababisha kilio.

Wanakandarasi wanalia kwamba, serikali haijawalipa mabilioni ya pesa na kuweka mali yao kwenye hatari ya kupigwa mnada.

Miradi hiyo imezua utata, hasa katika miji ya Nairobi, Kisumu, Nakuru na Mombasa ambako wakazi wanatimuliwa katika mitaa inayolengwa kwa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Katika kisa cha hivi punde, wakazi wa mtaa wa Woodley Estate, Nairobi, wanapinga mpango wa kuhamishwa kwa wapangaji 43 ili kutoa nafasi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu chini ya mpango mkubwa wa serikali ya Kenya Kwanza.

Serikali inakata ushuru wa asilimia 1.5 kwa mishahara ya wafanyakazi wote nchini wanaosema ni wa kufanikisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Uwezekano wa kunufaika ni finyu

Rais William Ruto akiweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa nyumba 2,384 za bei nafuu katika mtaa wa Lumumba, Kisumu Central, kaunti ya Kisumu.
Ubomoaji wa makazi kupisha nyumba hizo za bei nafuu umezua kilio kwa wengi. Picha|PCS

Hii ni licha ya uwezekano wa wengi wao kunufaika na nyumba hizo kuwa finyu sana.

“Hatua ya serikali ya kaunti inakiuka haki zetu za kumiliki mali. Hatukushauriwa kuhusu ubomoaji wa nyumba zetu. Huu ni mpango wa watu wenye ushawishi wa kunyakua mali yetu. Hatutakubali hatua hiyo,” Joseph Kang’ethe, mkazi wa mtaa wa Woodley.

Lakini Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alihakikisha kuwa watarejeshewa nyumba yao mara tu baada ya ujenzi kukamilika.

Serikali inapanga kujenga jumla ya nyumba 10,000 katika mitaa ya Bahati, Jericho, Lumumba, Maringo, Woodley. Ziwani, Embakasi, Kariobangi Kaskazini na Bondeni.

Haya yanajiri huku sekta ya ujenzi ikipata pigo kubwa kufuatia ongezeko kubwa la gharama ya vifaa vya ujenzi, na kusababisha uhaba mkubwa wa vifaa humu nchini.

Kupanda kwa bei za vifaa hivyo kumeathiri miradi inayoendelea ya wizara na idara za serikali huku wakandarasi wakitaka gharama ichunguzwe upya ili kuakisi bei ya sasa.

Wakandarasi hao wamelaani kupanda kwa kasi kwa gharama ya chuma aina ya T25 ikipanda kutoka Sh5,000 hadi Sh7,000 na T16 ikipanda hadi Sh1,600 kutoka Sh1,100.

Wanadai kuwa hii imekuwa na athari hasi kwa ujenzi.

Gharama ya vifaa vya ujenzi

“Gharama ya vifaa vingi ikiwa ni pamoja na simiti, chuma, mbao na rangi imepanda sana jambo ambalo huenda likawalazimu wanakandarasi wengi kubadilisha gharama ya miradi inayoendelea ya serikali ya kitaifa na kaunti,” alisema Clement Bowen wa kampuni ya ujenzi ya Bowen.

Wanakandarasi hao jana walisema wako katika hatari ya mali yao kupigwa mnada kwa kukosa kulipwa na serikali za kaunti na ya kitaifa.

Baadhi yao wamepokea notisi kwa taasisi za kifedha walipe au mali yao ipigwe mnada.

“Tunakumbwa na hatari ya mali yetu kupigwa mnada na benki na ili kurejesha pesa zao. Hata kampuni ambazo zilikuwa imara sasa zinajipata pabaya kwa sababu ya serikali kukosa kuwalipa,” akasema Clement Chebet, mmoja wa wanakandarasi.

Inakadiriwa kuwa kampuni hizo zinadai serikali ya kitaifa na za kaunti Sh300 bilioni.

“Serikali inafaa kutoa hakikisho kwa taasisi za kifedha kuhusu ni lini itatulipa pesa zetu badala ya mali yetu kupigwa mnada,” alisema Kemboi Kemei, mwanakandarasi mwingine kutoka mjini Eldoret.

Alifichua kuwa wengi wa wakandarasi na wasambazaji bidhaa hupata mikopo kutoka kwa benki za kibinafsi ili kufanya biashara na serikali lakini kucheleweshwa kwa malipo kunaathiri shughuli zao.

“Mikopo hiyo inaendelea kuvutia riba ambayo huenda ikatufanya tukapoteza mali zetu kwa madalali iwapo hatutalipwa madeni,” alisema Bw Kemei.

RIPOTI ZA BENSON MATHEKA, ERIC MATARA NA BARNABAS BII