MakalaMaoni

Serikali inaweza kurekebisha makosa yake mengi kwa kuheshimu katiba

Na BENSON MATHEKA November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KUMEKUWA na maswali kuhusu ni kwa nini serikali ya Kenya Kwanza inafanya makosa ya wazi kama kutetea mikataba ya kampuni ya Adani kutoka India ambayo ililaumiwa kwa mbinu zake za kupata kandarasi za mabilioni katika mataifa mengi ulimwenguni.

Wanaofahamu jinsi serikali inavyofanya kazi wanauliza iwapo ni washauri wa serikali wanaoipotosha au ni viongozi wanaopuuza ushauri ikizingatiwa imeajiri baada ya wataalamu wenye tajiriba pana katika sekta mbali mbali.

Kinachoatua moyo ni kuwa licha ya baadhi ya sera za serikali kuonekana wazi kutofaulu au kutangazwa kuwa kinyume cha katiba, serikali inazishinikiza na kuacha maswali kuhusu lengo la wanaozianzisha.

Kinachojitokeza hapa ni kwamba baadhi ya mipango na miradi inayozua utata hainuiwi kufaidi mwananchi wa kawaida mbali ni biashara ya watu binafsi wanaotumia ushawishi wao kuificha katika sera za umma.

Kama ingekuwa inanuiwa kufaidi raia, serikali haingekuwa inapuuza maoni na kilio chao.

Hii ndiyo sababu watu wanaolenga kunufaika nayo wanafanya kila wawezalo kuhakikisha imefanikiwa.

Kutimiza malengo yao wanatoa ushauri unaofedhehesha serikali wakati nchi zenye nguvu zinapoanika ukora wa kampuni kama Adani na wakati vijana wanapomwagika barabarani kulalamikia kuongezwa kwa ushuru unaofanya maisha yao kuwa magumu.

Iwapo sio washauri wanaopotosha viongozi basi ni viongozi ambao wanachangia hali za kufedhehesha ambazo zimekuwa zikishuhudiwa nchini chini ya utawala wa Kenya Kwanza.

Hili ni jambo linaloweza kurekebishwa na kurejesha heshima na hadhi ya nchi.

Inaweza kurekebishwa kwa kuepuka kukita maslahi ya kibinafsi katika miradi na mipango ya serikali, kushirikisha umma kikamilifu bila kuwa na maamuzi tayari, kuheshimu utawala wa sheria na katiba na kuruhusu ukosoaji chanya