Kitendawili cha vijana walioacha uhalifu kunyakua ardhi ya umma na kuigeuza jaa la taka
VIJANA 60 walioacha uhalifu na kuanza kukusanya taka kutoka eneo bunge la Dagoretti Kaskazini na Kusini wanalaumiwa kwa kunyakua ardhi ya umma, kuigeuza jaa la taka na kuzuia ujenzi wa barabara ya Salim.
Wakazi wa eneo hilo wanadai taka hizo ambazo zimetupwa na kundi la vijana hao ambao wanafahamika kama Strong Boys, zimekuwa kero zaidi kwa kusababisha maradhi na kurejesha nyuma maendeleo bila kujali wanaoishi katika eneo hilo.
Mkazi Bw Ali Njoroge, alisema ardhi hiyo ilianza kutumika miaka 30 iliyopita baada ya vijana waliorekebika tabia kukusanya taka kutoka kwa nyumba za kukodi ili kuepuka uhalifu.
Mwaka 2010 wakati wa kutekeleza ugatuzi chini ya Katiba mpya nchini, baadhi ya wakazi walichochea ardhi hiyo kutumika kujenga ofisi za umma kwa kuandamana, watu binafsi wakijitokeza kupinga.
“Wakati huo, Dagoretti Kaskazini hatukuwa na ofisi ya Mbunge, tulipendekeza ijengwe kwenye ardhi hiyo lakini kukawa na pingamizi kutoka kwa watu binafsi. Hivi sasa kila mbunge anayechanguliwa anafanyia shughuli huko Lavington,” alisema Njoroge.
Bw Njoroge alisema wakati wa mikutano ya umma na maandamano iliyofanywa na wakazi, kuna mmiliki mmoja wa nyumba katika mtaa huo alijitokeza akidai kumiliki ardhi hiyo.
“Mmiliki huyu alikataa ofisi kujengwa kwenye ardhi hiyo,” aliongeza.
Pingamizi hilo lilitoa mwanya mwingine kwa vijana wa Strong Boys kuendelea kutupa taka, jambo ambalo Bw Zainabu Osman anasema kuwepo kwa ushirikiano kati ya vijana na wamiliki wa ardhi.
Bi Osman alikosoa maafisa wafisadi kutoka serikali ya Kaunti ya Nairobi ambao wanachangia ardhi hiyo kubaki eneo la taka. Aliongeza kuwa licha ya juhudi za Serikali ya Kaunti kutuma wafanyakazi wake kuzoa taka, malori ya kaunti husalia hapo kwa muda mrefu bila kuondoa taka hiyo.
“Yanapopangana hapa, huwa tunatarajia taka zote ziondolewe. Kuna uvumi kwamba wanalipwa Sh5,000 ili wasiondoe taka. Ikiwa taka zitaondolewa, wana wasiwasi na nafasi ya maendeleo itapatikana,” alisema Bw Osman.
Madai hayo yalikanushwa vikali na mmiliki aliyeshutumiwa kufadhili malipo ya kuhakikisha vijana wanabaki katika eneo hilo.
Kulingana na Bw Hassan Omar, alitoa wazo la kipande hicho kutumika miaka 30 iliyopita baada ya kuona vijana wengi mtaani wakihangaika walikijihusisha na uhalifu.
Vijana kuasi uhalifu
Kwa wakati huo, Bw Omar alipendekezea vijana hao kuasi uhalifu na badala yake waanze kukusanya taka ya kuwapa kipato.
“Ardhi hiyo haikuwa yangu; nilipendekeza tu wazo hilo kwa sababu niliwaona vijana hao wakitusumbua. Unapoliangalia eneo hilo, kuna mtu anadai kuwa ni ardhi yake, lakini ilikuwa ardhi iliyotengwa kuwa makaburi ya umma,” alisema Bw Omar.
“Kuna madai nachangia kuzuia kuondolewa kwa taka hizo ambayo si kweli. Serikali ina wajibu wake, na vijana wanao wao. Na nilipotoa pendekezo langu, sina tena jukumu lolote kwa kinachoendelea,” alijitetea Bw Omar.
Kiongozi wa kundi la Strong Boys Bw Dominic Maradi, anasema wataendelea kukalia ardhi hiyo bila kuzuia ujenzi wa barabara ya Salim.
Alisema vijana wake 60 wataendelea kutupa taka kama kitega uchumi baada ya viongozi waliowachagua kuwatelekeza.
“Mwaka 2022 na 2023, tuliona magari ya kuchimba barabara hapa. Tulikubali waendelee kuanzisha ujenzi wa barabara ambayo tuliamini pia sisi tutanufaika. Baada ya siku tatu hayakuwa tena,” alisema Bw Maradi.
Kiongozi huyo alisistiza kuwa hawataruhusu mamlaka kuwaondoa kwenye ardhi ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya ofisi za umma.
Alipinga sehemu hiyo kufungwa akilaumu maafisa wafisadi ambao wanahusika katika shughuli ya kufunga. Alisema ukusanyaji taka hizo umemwezesha kupata pesa ambazo anakimu familia yake.
“Wakati malori yanakuja kuchukua taka, sisi hatuhusiki. Tunajua ardhi hii ni ya umma lakini kuna mtu anayejidai kumiliki, tunataka ajitokeze kwa kutoa nyaraka sahihi za ardhi hii,” aliongeza Maradi.
Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi, aliwaomba vijana hao wakusanye taka hizo na kuhakikisha zinapelekwa hadi eneo la Dandora, akiwataka pia, kuhakikisha taka hizo hazizuii barabara za umma kujengwa.
“Hawa ni vijana ambao, ukiwazuia kufanya hivi, wanaweza kuanza wizi. Inasikitisha kuona taka zikizuia ujenzi wa barabara. Natoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha taka hazizuii mradi wowote,” alisema Bi Elachi.
Afisa Mkuu wa Mazingira katika Kaunti ya Nairobi Bw Geoffrey Mosiria, alitaja eneo hilo la taka kuwa haramu. Alilaumu vijana na wamiliki wa ardhi kwa kuzuia ofisi yake na NEMA kutekeleza jukumu la kulifunga. Afisa huyo alisema taka zinazotupwa katika eneo hilo zinakiuka sheria za mazingira za kitaifa.
“Eneo hilo linasimamiwa na baadhi ya watu wafisadi. Ofisi yangu inataka wakazi wapumue hewa safi, lakini watu hao wamezuia. Pili, viongozi wao wanadai kuwa linawapa pesa,” aliteta.
Katiba ya Kenya chini ya Sheria ya Usimamizi na Uratibu wa Mazingira Sehemu ya 10, inaeleza kuwa mtu yeyote aliye na leseni ya kutupa taka, lazima atimize masharti yote yaliyowekwa na Mamlaka ili kuhakikisha kuwa eneo hilo la kutupa taka au mmea linaendeshwa kwa njia inayozingatia mazingira.
Athari za kutupa taka katika maeneo haramu
Katika mtaa huo ulio na wakazi zaidi ya 50,000 utupaji wa taka hizo unawavunja moyo wengi wakikabiliana na maradhi ya kipindupindu kila mara.
Mfanyabiashara na mpangaji Bw Yusuf Waidhanji alisema amewapoteza wateja wengi waliokuwa wakinunua chakula kutoka kwake, baada ya kulalamika kuongezeka kwa nzi na kuharisha kila wakati.
“Kila wakati wanapokuja kuchukua taka, inaongezeka maradufu kuliko awali. Siku inayofuata, watu wanaanza kuharisha,” alisema Bw Waidhanji.
Aliiomba serikali ya kaunti kutumia taka hiyo kuzalisha nishati ili kuboresha mazingira safi.
“Mwanangu anashindwa kupumua na hatuna uwezo wa kuhamia kwingine,” aliongeza Waidhaji.
Kwa upande mwingine, wamiliki wa nyumba wanaendelea kupata hasara kwani wapangaji wanahamia kwingine kutokana na harufu isiyovumilika. Bi Njoki Kamau 57, alisema zaidi ya nyumba zake 60, ambazo alichukua mkopo miaka miwili iliyopita, zimeachwa bila wapangaji.
“Wakazi wengi wameondoka kutokana na harufu isiyovumilika na hatari zinazoongezeka za kiafya. Ninapoteza Sh3000 kwa kila nyumba tupu kila mwezi. Serikali ya kaunti inakataa kushughulikia hili,” aliongeza Kamau.
Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA), Kaunti ya Nairobi huzalisha kati ya tani 2,000 hadi 2,500 za taka kila siku, ambapo taka hizo asilimia 80 ni za kikaboni na asilimia 20 ni za plastiki.