Habari za Kitaifa

Tungezuia Gachagua asivamiwe lakini hatukuwa na habari- DCI

Na MWANGI MUIRURI November 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

MKURUGENZI wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin amesema ukosefu wa habari za kijasusi ndio ulichangia maafisa wake kutotibua shambulio katika hafla ya mazishi iliyohudhuriwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua Limuru, Kiambu, Alhamisi.

Bw Gachagua, aliyelaumu serikali kwa kuchochea fujo kwa nia ya kumuua, alikuwa amehudhuria mazishi ya Erastus Nduati, 23, katika kijiji cha Bibirion.

Japo, hakujeruhiwa katika fujo hizo, gari lake liliharibiwa baada ya kushambuliwa kwa mawe na viti.

Drama nyingine ilitokea ambapo aliyekuwa Mbunge wa Limuru Peter Mwathi na Diwani wa Wadi ya Bibirioni Christopher Ireri walidai walitekwa nyara katika eneo la tukio na kusukumwa ndani ya magari ya Subaru, wakazungushwa kabla ya kutelekezwa karibu na mji wa Ruiru.

“Kisa cha Alhamisi kilichotokea eneo la Limuru kinachunguzwa na hatua kamili itachukuliwa dhidi ya wahusika wote,” Bw Amin akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu jana.

Mkurugenzi huyo wa DCI aliwashauri wahusika wote kukoma kutoa madai ambayo hayajawasilishwa rasmi katika vituo vya polisi.

“Ikiwa unadai kuwa umetekwa nyara, tafadhali wasilisha ripoti kwa kituo cha polisi ili tuanzishe uchunguzi. Ikiwa uliwaona wavamizi hao au unayo habari ambazo zinaweza kutusaidia kuwanasa wahalifu hao, ziwasilishe kwetu. Hatupendelei upande wowote na tumejitolea kudumisha utawala wa sheria,” Bw Amin akasema.

Akaongeza kwamba “hatukuwa na habari zozote kuhusu mipango ya watu fulani kutekeleza shambulio hilo.”

Hata hivyo, Bw Gachagua alielekeza kidole cha lawama kwa wandani wa Rais William Ruto, ambao hakuwataja majina.

Alidai kuwa watu hao wamejitolea kulifanya eneo la Mlima Kenya kuwa ngome ya fujo ili kuficha kile ambacho alitaja kuwa serikali kupoteza uungwaji mkono.

“Mnamo Jumanne Rais alikemea kile alichokotaja kama ukabila, chuki na kutovumilia. Lakini sasa wandani wake katika Lamu na Kiambu wamemkaidi kuwa kutoa matamshi ya chuki na kushiriki fujo. Amejivuta kukemea maovu kama hayo,” Bw Gachagua akaambia Taifa Leo.

Naibu huyo wa rais wa zamani alikuwa akirejelea kanda ya video inayozungushwa katika mitandao ya kijamii ikimwonyesha Mkurugenzi wa Shirika la Kiislamu la Kutetea Hazi za Kibinadamu (Muhur) Khelef Khalifa akisema kaunti ya Lamu sio ya jamii ya Agikuyu na hivyo hawafai kumiliki ardhi au kuwania nyadhifa.

Bw Khalifa ameshikilia kuwa hataomba msamaha kwa kutoa kauli kama hizo za kuchochea chuki.

Mwanaharakati huyo sasa ameagizwa kufika mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kuhojiwa kuhusu matamshi hayo ya uchochezi.

Hata yanajiri huku ripoti moja ya Kamati ya Usalama katika Kaunti ya Kiambu iliyoonekana na Taifa Leo inasema kuwa ujumbe ulitumwa saa nne za asubuhi (10 am) ukionya kuwa magari sita yalionekana karibu na kampuni ya Limuru Dairies yakiwa na watu 80 wasiojulikana.

Licha ya onyo hilo kutolea, maafisa wa polisi hawakutumwa eneo hilo.

Na fujo zilipotokea Bw Gachagua, ambaye hana walinzi wa serikali, aliokolewa na walinzi wa kibinafsi ambao waliokodiwa kumlinda.

Badala yake, Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Kiambu Michael Muchiri aliambia Taifa Leo kwamba kisa hicho kinashughulikiwa na makao makuu ya polisi.

“Wasiliana na makao makuu ya polisi, jumba la Vigilance. Msemaji wetu (Dkt Resila Onyango) atakusaidia,” Muchiri akasema.

Taarifa kutoka makao makuu ya polisi kuhusu uchunguzi wa kisa hicho imetoa mwongozo kuhusu namna ya kutanzua kitendawili cha kushambuliwa kwa Gachagua.

“Maafisa wetu mashinani wameagizwa kukagua picha za kamera za usalama (CCTV) za eneo ambako uhalifu ulitokea, wawatambue washukiwa wakuu waliopanga na kufadhili shambulio hilo wakague kanda za CCTV zilizonaswa karibu na kituo cha matatu ambako inashukiwa wavamizi walishukishwa kutoka kwa magari kadhaa, watoe maagizo kwa watu waandikishe taarifa na wawahoji wakazi kupata habari zaidi kuhusu shambulio hili,” inasema taarifa hiyo.

Kufikia sasa Seneta wa Kiambu Karungo Thang’wa ameagizwa kufikia mbele ya Kamati ya Usalama eneo la Kati, mjini Nyeri, kuandikisha taarifa.

Mwanasiasa huyo amekosoa hatua hiyo akisema haina mantiki ikizingatiwa kuwa uhalifu ulitendeka Kiambu.

“Mimi na viongozi wenzangu tulikuwa tumeenda katika makao makuu ya DCI kupiga ripoti kuhusu shambulio hilo. Lakini baada ya maafisa hao wakiongozwa na bosi wao Mohamed Amin kukataa kutusikiza, tunaagizwa kuripoti katika makao makuu ya Kaunti ya Nyeri,” akasema.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA