Maoni: Kutekwa kwa Bunge na Serikali kumegharimu nchi heshima na fahari yake
UFICHUZI wa dili tata za Adani ambazo zilifutwa baada ya Amerika kuanika ufisadi wa wakuu wa kampuni hiyo, sakata ya mafuta ya kupikia ya mabilioni, ile ya mfumo wa Afya kwa Wote ya Sh104 bilioni na inayodaiwa kutibuka ya kueneza propaganda za serikali kusaidia Rais Ruto kuimarisha umaarufu wake, unaweza kuwa tone tu la kashfa zinazofanyika chini ya Serikali ya Kenya Kwanza.
Hii ni kwa sababu serikali imezima uangalizi wowote wa maana kwa kuweka wabunge makwapani hivi kwamba wanafumbia macho masuala muhimu hata raia wanapokandamizwa.
Isipokuwa dili ya Adani ya kutwaa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ambayo Kamati ya Bunge ilionekana kujivuta kuiidhinisha, nyingi ya kamati za bunge zimekuwa zikiitakasa serikali kwa mipango tata hata ikiwa ikikataliwa na raia.
Ikiwa wanaweza kupitisha mswada wa fedha wakati ambao ilionekana wazi kuwa ulikuwa umekataliwa na raia, ni nini ambacho hawawezi kupitisha wakitakiwa na serikali kufanya hivyo?
Ni wazi kuwa wabunge hawaulizi maswali mazito kila wakati serikali inapowasilisha sheria na mipango yake na wanachofanya ni kuitia muhuri bila kujali athari zake kwa raia na nchi kwa jumula.
Kwa kufanya hivi, si ajabu wameidhinisha kashfa nyingi za mabilioni ya pesa ambazo ziliingia kwa mifuko ya watu wenye ushawishi. Bunge ya sasa imegeuka kuwa kibaraka wa serikali na hii imegharimu nchi huku heshima na sifa ambazo imedumisha kwa miaka mingi zikimomonyoka haraka.
Kama wabunge wangefanya kazi yao ipasavyo, sakata hizi na zile ambazo hazijapata wa kuzifichua haziwezi kuwepo. Bunge la sasa lina wataalamu wa kila sekta ambao wamekubali kutumiwa kuharibu nchi yao.